LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 26, 2019

TAKWA NA KUZUIA MAENDELEO YA MAKOMBORA YA IRAN, NDOTO AMBAYO HAITATIMIA

Uwezo wa kijeshi wa Iran ikiwa ni pamoja na makombora yake ya balestiki vinatengenezwa kwa ajili ya kujilinda na kuhami nchi. Makombora na silaha hizo za kijihami zinatengenezwa kwa nmna ambayo hazina uwezo wa kubeba vichwa vya mabomu ya nyuklia.
Pamoja na hayo Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya zinafanya jitihada za kuanzisha hujuma ya vyombo vya habari dhidi ya miradi ya kutengenza makombora hapa nchini kwa kutumia sera maarufu ya hujuma na propaganda chafu za kutaka kuidhihirisha Iran kuwa ni tishio katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika fremu ya sera hizo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian amekariri madai yasiyo na msingi dhidi ya miradi ya kutengeneza makombora ya Iran na kutoa wito wa kusitishwa utengenezaji wa makombora ya balestiki hapa nchini. 
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi amejibu madai hayo kwa kusisitiza kuwa, uwezo wa makombora ya Iran ni sehemu ya nguvu halali ya kujihami na kulinda usalama wa Jamhuri ya Kiislamu. Qassemi amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inajipanga katika masuala ya ulinzi kwa mujibu wa tathmini yake halisi kuhusu vitisho vinavyoikabili na itaimarisha uwezo huo kadiri inavyohitajika.
Bahram Qassemi
Tofauti ya madai yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, miradi ya kutengeneza makombora ya Iran haikinzani na sheria za kimataifa wala azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kuhusu azimio hilo inatupasa kuashiria nukta mbili. Kwanza ni kwamba, tofauti na azimio la kabla yake yaani azimio nambari 1929, azimio hilo limetumia lugha isiyo ya kulazimisha kuhusu miradi na majaribio ya makombora ya Iran. Pili ni kwamba, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN linaitaka Iran isizalishe makombora ya balestiki yanayoweza kubeba vichwa vya silaha za nyuklia.  
Katika mazungumzo yake na televisheni ya al Jazeera ya Qatar, Gareth Porter mwandishi na mchambuzi wa Kimarekani ameashiria sera za ulinzi za Iran na jinsi Tehran ilivyojiepusha kutengeneza za silaha za nyuklia na kusema: "Ni wazi kuwa, Iran inatumia makombora ya balestiki kama silaha ya kujihami hasa kwa kutilia maanani kwamba, Israel na Saudi Arabia zina makombora ya balestiki yanayoweza kutumiwa kuishambulia Iran. Kwa msingi huo makombora ya balestiki ya Iran ni kwa ajili ya kujihami na kujilinda."
Kombora la balestiki la Iran
Kukaririwa kwa madai haya na baadhi ya nchi za Ulaya ni kielelezo kwamba, lengo lao ni kuendeleza misimamo ya Marekani ya kutaka kuiarifisha miradi ya makombora ya Iran kuwa ni hatari kwa eneo la Mashariki ya Kati na siasa hizo zinagongana na ni za hadaa na ghilba. Hapana shaka kuwa, lengo la madai kama haya ni kutaka kudhoofisha uwezo wa kujihami wa Iran. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, uwezo wa makombora ya Iran ni nguzo muhimu sana ya usalama na amani ya nchi hii. Hasahasa kwa kutilia maanani kwamba, nchi za Magharibi hususan Ufaransa na Marekani zimelifanya eneo hili la Mashariki ya Kati kama ghala kubwa la silaha na aina mbalimbali ya makombora ya kisasa.
Inatupasa pia kuashiria kwamba, msimamo wa Ufaransa kuhusiana na kadhia hii unapaswa kupewa mazingatio maalumu. Kutokana na matatizo yake ya ndani, Paris imeonesha hamu kubwa ya kutaka kufuata na kuwa bega kwa bega na Marekani na inahitajia sana kuuza silaha kwa nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemii. Haya yote yanachangia katika misimamo kama hii ya serikali ya Paris kuhusu uwezo wa makombora wa Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alisema katika kumbukumbu ya mwaka wa 29 tangu Imam Ruhullah Khomeini aage dunia kwamba: "Katika kipindi cha vita vya kulazimishwa na kutokana na kwamba, Iran haikuwa na silaha wala makombora ya kuweza kujihami, kuanzia miji ya mpakani hadi Tehran ilikuwa ikishambuliwa kwa makombora usiku na mchana, lakini hivi sasa na kutokana na hima na jitihada kubwa za wataalamu vijana, Iran imekuwa nguvu ya kwanza ya makombora katika eneo la Mashariki ya Kati na adui anajua vyema kwamba, iwapo atapiga kombora moja atajibiwa kwa makombora kumi."
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu
Akiashiria matamshi ya baadhi ya viongozi wa nchi za Ulaya, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Inaonekana kuwa, nchi hizo zinatarajia kwamba, taifa la Iran litavumilia vikwazo, miradi yake ya nishati ya nyuklia ambayo ni muhimu sana kwa mustakbali wa Iran ifungwe na vizingiti ilivyowekewa viendelee; hata hivyo tunawaambia kuwa, ndoto hii ya mchana kamwe haitatimia."  

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages