Aguila Saleh Spika wa bunge la Libya lenye makao yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi amesema kuwa nchi hiyo lazima iendelee mbele na chaguzi za kitaifa hata kama wapiga kura watapinga rasimu ya katiba katika kura ya maoni inayopangwa kufanyika nchini humo.
Umoja wa Mataifa na nchi za magharibi zinataraji kuwa Libya itaendesha chaguzi zake za kitaifa ifikapo mwezi Juni baada ya kuendesha kura ya maoni kuhusu katiba ya nchi hiyo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo uliojitokeza baada ya kupinduliwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi mwaka 2011.
Akizungumza na shirika la habari la Reuters katika mji anakotoka wa Qubba mashariki mwa Libya; Agula Saleh amesema kuwa wanataka wapate katiba kwa mujibu wa mapatano yatakayofikiwa na kwamba jambo hilo litachukua tamu. Amesema wanahitaji kuwa na mamlaka ya utendaji na kwamba hakuna chaguo jingine isipokuwa kumchagua mwenyekiti wa muda kama rasimu hiyo ya katiba imepingwa. Itakumbukwa kuwa Libya ina serikali mbili; moja ikiwa katika mji mkuu Tripoli na moja ikiwa na makao yake mashariki mwa nchi ambayo ina mfungamano na kamanda Khalifa Haftar ambaye vikosi vyake vinayashikilia maeneo ya mashariki mwa Libya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇