JANA Disemba 16, 2019 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Dkt. Olusegun Obasanjo Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Dkt. Obasanjo amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika uongozi wake ikiwemokupambana na rushwa, kuimarisha utoaji wa elimu, kuimarisha miundombinu, kuongeza nishati ya umeme, kuboresha usafiri wa ardhini na angani na jinsi wadau mbalimbali wa ndani na nje wanavyopaswa kuelewa juhudi zinazofanyika.
Mhe. Dkt. Obasanjo alisema Mhe. Rais Magufuli amedhihirisha kuwa kiongozi imara wa kusimamia mambo muhimu yenye maslahi kwa nchi yake na amebainisha kuwa licha ya kwamba maendeleo ya nchi hayapatikani mara moja lakini kwa muda mfupi Mhe. Rais Magufuli amefanya juhudi kubwa za kuimarisha maeneo ya huduma za kijamii, kukiimarisha chama chake cha siasa (Chama Cha Mapinduzi – CCM) na kwamba ameonesha kuwa anakijua anachokifanya katika maeneo ya uchumi.
“Tusijisahau kwamba ukoloni mamboleo bado upo na mabeberu bado wanaendelea kufanya juhudi za kuhakikisha wanatunyonya, na kiongozi yeyote wa Afrika anayethubutu kuwazuia hawezi kuwa rafiki wa hao ambao walikuwa wakinufaika kwa kutunyonya”alisisitiza Mhe. Dkt. Obasanjo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇