Rais Dkt. John Magufuli leo amefanya mazungumzo na viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya Dini hapa nchini na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa wa kutoa huduma za kiroho na kijamii kupitia taasisi wanazoziongoza.
Mkutano umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Jumaa Aweso.
Akizungumza baada ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo ya viongozi hao wa Dini, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Madhehebu ya Dini katika kuihudumia jamii na ameahidi kuwa itaendeleza ushirikiano huo mzuri kwa kuwa una manufaa makubwa kwa wananchi na katika ujenzi wa Taifa.
Rais Magufuli ameahidi kuwa Serikali itafanyia kazi maoni, ushauri na mapendekezo yote yaliyotolewa na viongozi hao wa Dini, na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo kuongeza usambazaji wa maji kwa wananchi, kujenga miundombinu ya elimu, afya na usafiri, kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi hadi sekondari, kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa vyuo vya Serikali na visivyo vya Serikali na kulinda amani na usalama wa nchi.
Kuhusu usimamizi wa ubora wa huduma zinazotolewa na baadhi ya taasisi zilizo chini ya Madhehebu ya Dini kama vile vyuo na hospitali, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali inachukua hatua hizo ili kuhakikisha Watanzania wanapata elimu na matibabu bora kwa gharama nafuu, na kwamba haifanyi hivyo kwa lengo kuziumiza taasisi hizo.
Kwa upande wa misamaha ya kodi, Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali haijafuta misamaha ya kodi kwa taasisi za Dini huku akibainisha kuwa mwaka 2016 ilitoa misamaha yenye thamani ya shilingi Bilioni 19.66, mwaka 2017 ilitoa misamaha yenye thamani ya shilingi Bilioni 17.6 na mwaka 2018 ilitoa misamaha yenye thamani ya shilingi Bilioni 46.84 na kwamba pamoja na kutoa misamaha hiyo kumekuwa na changamoto ya baadhi ya taasisi kuuza bidhaa zinawekewa misamaha ama kutumia bidhaa za misahama ya kodi kufanyia kibiashara.
Kuhusu zoezi la uhakiki wa wakulima wa korosho kwenda polepole na hivyo kusababisha wakulima wengi kutolipwa fedha zao, Mhe. Rais Magufuli amewaagiza viongozi wa Mikoa, Wilaya na Tarafa kuondoa urasimu katika uhakiki huo na hivyo kuharakisha zoezi ili wakulima walipwe mapema kwa kuwa fedha za malipo ya korosho zao zipo.
Mhe. Rais Magufuli amekubaliana na maoni ya viongozi wa Dini kwa kuwataka viongozi wa Serikali katika ngazi mbalimbali kuweka utaratibu wa kukutana na kuzungumza na Viongozi wa Madhehebu ya Dini katika maeneo yao, na amemuagiza Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa kuhakikisha kero za Viongozi wa Dini zinatatuliwa.
Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amesema Serikali itafanyia kazi ushauri wa kudhibiti michezo ya kamali ambayo inazidi kushika kasi na kusababisha wananchi hasa vijana kutumia muda mwingi kucheza kamali badala ya kufanya kazi za uzalishaji mali kwa ajili ya ujenzi wa Taifa.
Pamoja na kutoa maoni hayo viongozi hao wa Dini wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake mzuri, uzalendo, ukweli na kutekeleza kwa vitendo ahadi alizozitoa kwa Watanzania, na wamemuahidi kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali anayoiongoza na kumuombea.
Your Ad Spot
Jan 23, 2019
Home
Unlabelled
RAIS DK. MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA DINI NCHINI, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM, LEO
RAIS DK. MAGUFULI AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA DINI NCHINI, IKULU JIJINI DAR ES SALAAM, LEO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇