LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 30, 2019

SERIKALI YAPONGEZWA NA WADAU KWA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA TANESCO



NA K-VIS BLOG/Khalfan Said, KIA
HATUA ya Serikali ya Awamu ya Tano, ya kuliwezesha Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kuboresha miundombinu yake ya umeme imepongezwa na wawekezaji mbalimbali kwenye mkoa wa Kilimajaro na Arusha kwani kumeongeza tija katika uzalishaji lakini pia kuboresha utoaji huduma.

Serikali kupitia Shirika lake la Umeme, TANESCO  ilifanya kazi kubwa ya kukarabati na kuboresha miundombinu ya umeme ikiwemo, njia za kusafirisha umeme, lakini pia vituo vya kupoza na kusambaza umeme kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha kupitia mradi wa TEDAP.

Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha KIA, ni moja ya vituo vipya vilivyojengwa kupitia mradi huo na kimekuwa nguzo kubwa ya kutoa huduma bora ya umeme kwenye mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Akielezea manufaa ya kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni iliyopewa kandarasi ya kusimamia shughuli za uendeshaji wa Kiwanja  cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro KIA, ijulikanayo kama KADCO, Mhandisi Christopher Andendekisye Mukoma alisema, sehemu kubwa ya utoaji huduma kwenye kiwanja hicho kunategemea umeme, na sio tu umeme bali umeme wa uhakika.

“Kituo cha kupoza umeme cha KIA, ambacho kiko kama kilomita nne kutoka hapa, kimeondoa kabisa tatizo la umeme tulilokuwa nalo kwa muda mrefu,” alisema Mhandisi Mukoma.

Tulilalamika sana kwa viongozi wa serikali kuhusu tatizo la umeme, lakini  tunashukuru serikali ya awamu ya tano ilisikiliza kilio chetu na hivyo kuboresha miundombinu ya umeme na kwa hakika hata gharama za uendeshaji katika eneo la umeme zimeshuka kwa asilimia 50.” Alibainisha.

Sio hivyo tu, kiwanja hiki kilikuwa kikihudumia abiria 500 kwa mwaka, lakini hivi sasa tunahudumia abiria kati ya milioni 1 hadi milioni 2 kwa mwaka na moja ya sababu ni kuwa na umeme wa uhakika.” Alisema.

Akieleza umuhimu wa umeme kwenye shughuli za uendeshaji kiwanja cha ndege Mhandisi Mukoma alisema, rubani anapotaka kutua usiku, na tayari ameshafanya maandalizi ya kutua, umeme ukikatika kwenye run way (njia ya kutua ndege) basi sheria na kanuni zinamtaka ahesabu sekunde nane, zikiisha kama bado haujarejea tena, basi anatakiwa aachane na mpango wa kutua na hivyo kupaa tena na hii ni hatari.” Alisema

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha Harsho Group, kilichoko eneo la kijiji cha kwa Sadala, Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro, Bw. Harold A. Shoo alisema, huduma ya umeme itolewayo na TANESCO kwa sasa imeboreka kwa kiwango kikubwa.

“Tulianza tukiwa na shida kubwa ya low voltage (umeme mdogo) na power cut (umeme kukatika), kwenye miaka ya 2016/2017 na tulikuwa end user wa umeme wa HT ambao ulikuwa unazunguka kwenye eneo kubwa, lakini kupitia sub station ya KIA, na sisi tumenufaika kuanzia 2018 hadi sasa tumekuwa tukipata umeme frequently (muda wote) nikiri kusema huduma ya umeme kwa sasa ni bora.” Alisema

Alisema, kiwanda chake kinalipa bili ya umeme kiasi cha shilingi milioni 35 hadi 45 kwa mwezi na amekuwa mlipaji mzuri na kwa kipindi chote hajawahi kuingia kwenye mgogoro na TANESCO kuhusu malipo ya bili.

Akizungumzia ajira kiwandani hapo, Bw. Shoo alisema, “Tumeajiri wafanyakazi wa kudumu kiasi cha 120 na vibarua 55 na kwakuwa tunapanua kiwanda, tumekusudia kuwa na shifti mbli usiku na mchana kwa hiyo tunaweza kufikia idadi ya wafanyakazi 200 wenye ajira ya kudumu.” Alisema.

Naye Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hezron S. Nganoga, ambaye ni Mkuu wa kiwanda cha viatu Karanga, ambacho kiko chini ya kampuni ya Karanga Leather Industries Limited, kinachomilikiwa kwa ubia kati ya Magereza na Mfuko wa Pensheni wa PSSSF, alipongeza juhudi za kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwani hivi sasa hawana tatizo lolote la umeme, kwani umeme unapatikana wakati wote na unatosheleza mahitaji ya kiwanda.

“Umeme tunaoupata kwa sasa hauna matatizo, hapo nyuma shida ilikuwepo, umeme ulikatika mara kwa mara, wakati mwingine sababu ya mvua au upepo, lakini kwa kiasi kikubwa TANESCO mmejitahidi sana, kwa jinsi mnavyoenda na maboresho mnayofanya yana tija kubwa kwa taifa.” Alisema.

Alisema, kiwanda kinakusudia kufanya upanuzi kwa hivyo TANESCO kama mdau mkubwa ajiandae kupokea maombi ya kuongezewa umeme.

Naye Meneja Mkuu wa kiwanda cha kutengeneza transfoma kinachomilikwia kwa ubia kati ya serikali na kampuni moja ya Kenya TENELEC kilichoko jijini Arusha, Bw.Zahir Saleh, alisema tangu mwaka 2018 hadi sasa upatikanaji wa umeme wa uhakika umekuwa bora sana.

“Hali ya umeme nikilinganisha na miaka ya 2015/2016 kwakweli kuna tofauti, ilifika mahala kwa mwezi mmoja lazima siku kumi tutumie umeme wa jenereta, lakini tangu 2017/2018 na sasa hali imeboreka sana.” Alisema.

Lakini si hivyo tu wafanyakazi wa TANESCO pia wanatupatia ushirikiano unaohitajika, hata pakitokea tatizo la umeme hapa kiwandani kwetu, wamekuwa wakitutumia wataalamu na wanashirikiana na wataalamu wetu kutatua tatizo hilo kwa haraka, tukitoa taarifa response yao ni ya haraka, alisema Bw. Saleh.

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Emmanuel G. Manirabona, alisema nia ya Shirika ni kuhakikisha wateja na wananchi kwa ujumla wanapata huduma ya umeme wakati wote na lengo la ziara ya kutembelea wateja wa Shirika hilo ni kupata mrejesho baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali kupitia TANESCO ya kukarabati na kuboresha miundombinu ya umeme kupitia mradi wa TEDAP.

Akizungumzia Mradi wa TEDAP ambao ulipelekea ujenzi wa kituo cha umeme KIA, Mhandisi Manirabona alisema, kabla ya mradi huo kulikuwa na laini ndogo za 33kv zilizokuwa zinatoka Moshi kwenye kituo cha umeme Kiyungi hadi Njiro jijini Arusha.

Alisema ililazimika kuangalia hali ya uzalishaji kwenye vituo hivyo viwili kama iko vizuri ndio waliweza kuleta umeme hapa, na hii ilileta shida kubwa ya umeme kwenye eneo hili, umeme ulikuwa low voltage na kwakweli iliyokana na safari kuwa ndefu ya kusafirisha umeme hadi kufikia mahala hapa, alisema Mhandisi Manirabora na kuongeza, kadiri mahitaji ya umeme yalivyoongezeka Serikali kupitia TANESCO ikaona upo umuhimu wa kujenga kituo kikubwa cha umeme KIA.

“Kituo hiki kina transfoma mbili kila moja ina Megawati 20 (20MVA) sawa na jumla ya Megawati 40 na wanaweza kusambaza na kulisha umeme kwenye maeneo ya Kilimanjaro, na Mirerani.

Aidha Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka alisema, “Kituo cha kupoza na kusambaza umemecha KIA kinahudumia eneo la Mirerani, kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha KIA ambao wanatumia Megawti 0.5, kiwanda cha Harsho Group kinatumia megawati kati ya 0.4 hadi 0.5, kiwanda cha vinywaji baridi Bonite Boatlas, kiwanda cha viatu Karanga, kiwanda cha maua, kiwanda cha Serengeti lakini pia wananchi kwa ujumla.” 
Alisema.

Kwa ujumla Mkoa wa Kilimanjaro pekee una miundombinu ya kupokea umeme wa  Megawati 120 ingawa mahitaji halisi ni Megawati 42 sawa na asilia 30 tu ya uwezo wa miundombinu ya umeme iliyoko Mkoani humo, alisema.
Miongoni mwa wateja wanaokusudia kuongeza uwezo ni kiwanda cha Biokim Ambao wataongeza Megwati 3 hii ni baada ya wawekezaji kuona hali yan umeme kwa sasa iko imara.


 Meneja Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Emmanuel G. Manirabona, akizungumza kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha KIA, Januari 25, 2019.
 Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, akifafanua baadhi ya mambo kuhusu umuhimu wa kituo hicho kwa wateja wa mkoa huo. Kushoto ni Meneja Mwasiliano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji.




 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni iliyopewa kandarasi ya kusimamia shughuli za uendeshaji wa Kiwanja  cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro KIA, ijulikanayo kama KADCO, Mhandisi Christopher Andendekisye Mukoma, akielezea upanuzi wa kiwanja hicho.
 Mifumo ya kupzoa hewa ya kiwanja cha KIA, ambayo hutumia kiasi kikubwa cha umeme.
 Mhandisi Christopher Andendekisye Mukoma.
  Mhandisi Christopher Andendekisye Mukoma akifafanua jambo mbele ya wahariri na waandishi wa habari wakiwemo watumishi wa TANESCO na wale wa KIA.


 Mfanyakazi wa kiwanda cha Harsho Group, akiwa kazini.
  Meneja Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO anayeshughulikia Miradi, Mhandisi Emmanuel G. Manirabona, akizungumza na Mkurugenzi wa kiwanda cha Harsho Group, Bw.Harold A. Shoo.
 Bw.Harold A. Shoo(kulia), akifafanua jambo mbele ya wahariri
  Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Mkaka, akizungumza kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Karanga Mkoani Kilimanjaro, kilichojengwa chini ya mradi wa TEDAP.
 Transfoma kubwa kwenye kituo cha kupoza na kusambvaza umeme cha Karanga .
 Mhandisi Manirabona, (kushoto), akizungumza na Mkuu wa Kiwanda cha viatu Karanga mkoani Kilimanjaro, 


Mrakibu Mwandamizi wa Magereza Hezron S. Nganoga. Aliyesimama ni  Afisi utawala Magereza Kilimanjaro, Mrakibu Msaidizi wa Magereza Hamisi Mnyaku

 Afisi utawala Magereza Kilimanjaro, Mrakibu Msaidizi wa Magereza Hamisi Mnyaku(kulia), akizunumza na Meneja wa TANESCO jiji la Arusha, Mhandisi Herini Mhina.



No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages