Serikali ya Tanzania imejitenga na kampeni ya kuwakamata na kushtaki mashoga inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania imeeleza kuwa, kampeni hiyo ni mawazo binafsi ya Paul Makonda na kwamba, si msimamo rasmi wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika taarifa hiyo, serikali ya Tanzania imesema kuwa, nchi hiyo itaendelea kuheshimu mikataba yote ya kimataifa ambayo imeisaini na kuiridhia sambamba na kuheshimu na kulinda haki kama zilivyo katika Katiba.
Tarifa hiyo ya aina yake ni ya kwanza kutolewa na Tanzania kuhusiana na masuala ya ushoga, na inaonesha taifa hilo kwa kiasi fulani limelegeza kamba juu ya vitendo hivyo, hasa kwa kutilia maanani kwamba, huko nyuma imewahi kukemea vitendo hivyo.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, serikali ya Tanzania imelazimika kutoa taarifa hiyo na kuonyesha kwamba, kampeni ya Paul Makonda si msimamo wa serikali ikihofia mashinikizo ya kimataifa na hata pengine kukatiwa misaada na baadhi ya madola ya kigeni yenye kuunga mkono mapenzi ya watu wa jinsia moja ya ushoga na usagaji.
Wakati huo huo, serikali ya Marekani imewaonya raia wake wanaoishi nchini Tanzania, kujihadhari baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalaam kutangaza operesheni ya kuwatafuta na kuwashtaki watu wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja. Taarifa hiyo imewashauri raia wa Marekani walioko Tanzania kupitia upya mitandao ya kijamii na kuondoa chochote kinachoweza kuwasababishia matatizo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇