Idadi ya watu waliopoteza maisha yao katika mashambulio ya kigaidi ya juzi katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu imeongezeka na kufikia 53.
Polisi ya Somalia imetangaza kuwa, hadi sasa watu waliopoteza maisha yao katika mashambulio hayo ya kigaidi wamefikia 53 na kwamba, kuna makumi ya wengine waliojeruhiwa katika tukio hilo ambao hali zao ni mbaya.
Mashambulizi hayo ya kigaidi ya siku ya Ijumaa yalilenga Hoteli ya Sahafi mjini Mogadishu, hoteli ambayo hutumiwa zaidi na maafisa wa serikali ya Somalia.
Ripoti zinasema magaidi kadhaa walishambulia hoteli hiyo iliyoko karibu na makao makuu ya Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai ya Somalia kwa magari kadhaa yaliyokuwa na mabomu na kuua makumi ya watu.
Kundi la kigaidi la al-Shabab limetangaza kuwa, limehusika na mashambulio hayo yya kigaidi.
Mashuhuda wanasema kuwa, vipande vya miili ya maiti waliouawa katika hujuma hiyo vilitapakaa huku na kule katika moja ya mashambulio mabaya kabisa kuwahi kuikumba Somalia katika miaka ya hivi karibuni.
Mwaka 2015 kundi la kigaidi la al-Shabab lilishambulia hoteli hiyo hiyo ya Sahafi na kuua wanasiasa na wabunge kadhaa wa Somalia.
Wapiganaji wa kundi la al-Shabab wamekuwa wakishambulia askari wa kikosi cha Umoja wa Afrika cha kulinda amani nchini Somalia, AMISOM na jeshi la Somalia.
Somalia ilitumbukia katika mapigano na machafuko ya ndani tangu ilipoondolewa madarakani serikali ya Mohamed Siad Barre mwanzoni mwa muongo wa 1990.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇