Na WAMJW – Ifakara
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Dini ya St.Francis kupunguza gharama za matibabu kwa wananchi ndani ya mwezi mmoja kabla hajarudi kufanya ukaguzi wa mara ya pili.
Ameyasema hayo wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya katika Hospitali ya St Francis iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Ifakara Mkoa wa Morogoro kufuatia taarifa isiyoridhisha juu ya gharama za matibabu iyoripotiwa siku ya Octoba 3 na Televisheni ya Taifa (TBC).
Waziri Ummy alisema kwamba, Serikali inatoa Jumla ya Watumishi 243 sawa na Asilimia 68% katika Hospitali hiyo, lengo ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini kupata huduma za bora za afya na zenye unafuu ikiwa ni moja kati ya ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli wakati anaingia madarakani.
“Kati ya Watumishi 352, watumishi 219 wanalipwa mshahara na Serikali Kuu, ambapo kila mwezi tunalipa shilingi milioni 153.7, bila kuhesabu gharama za watumishi 12 walioshikizwa kutoka Wizara ya Afya, Watumishi 12 kutoka Halmashauri ya Kilombero, Katibu tawala Morogoro ameleta watumishi 2, jumla watumishi 243, ambao ni sawa na Asilimia 68% wanalipwa mshahara kutoka Serikali kwa Asilimia 100%”. Alisema Mhe. Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa mwaka wa bajeti 2015/2016 Serikali ilipeleka dawa zenye thamani ya shilingi Millioni 119.5, bajeti ya mwaka 2016/2017 shilingi milioni 177.9 huku kwa mwaka 2017/2018 dawa zenye thamani ya shilingi milioni 118.7 zilinunuliwa hospitalini hapo.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy alisema kuwa mwongozo wa Wizara ya Afya, unazitaka Hospitali zote kuhakikisha kuwa wanawake wajawazito, wazee wasio na uwezo na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kupata huduma za matibabu bila malipo.
Mbali na hayo Waziri Ummy alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya bila kuwasahau watoto walio chini ya umri wa miaka 18 ambao hupata bima ya afya kwa shilingi 50,400/=
“Wakati umefika wa Watanzania kujenga utamaduni wa kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua, na uhakika huo ni wa kupitia Bima ya Afya”, alihimiza Waziri Ummy kwa msisitizo.
Waziri Ummy, aliendelea kusema kuwa, Serikali inaelekea kutunga sheria ambayo itamlazimu kila Mtanzania kupata Bima ya Afya, ili aweze kupata huduma za matibabu ya Afya bila kikwazo chochote cha fedha.
Naye Mbunge wa Jimbo la Kilombero Mhe. Peter Ambrose Lijualikali amemuomba Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu kuikumbuka Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero kwa kujenga Hospitali ya Wilaya, jambo litaloimarisha hali ya utoaji huduma za Afya kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya St. Fransis, Baba Askofu Salutaris Libena ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kufika hospitali hapo na kuahidi kutekeleza maelekezo yote ambayo yametolewa na Serikali.
” Tunaahidi kwamba tumeelewa na tutatekeleza maelekezo yote, katika lengo la kuboresha huduma za Afya kwa wananchi “, alisema Baba Askofu Libena.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇