Kwa akali raia 10 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameripotiwa kuuawa nchini Angola katika makabliano baina yao kwa upande mmoja na askari polisi na wananchi wa nchi hiyo jirani kwa upande wa pili.
Televisheni ya serikali ya Angola TPA imethibitisha kutokea mauaji hayo lakini inasisitiza kuwa, raia 10 wa Kongo pamoja na askari mmoja wa Angola wameuawa katika mapigano hayo yaliyotokea katika mji wa Lucapa mkoani Lunda Norte.
Hata hivyo Muungano wa Wakongomani wanaoishi Angola umesema raia 14 wa DRC wameuawa katika mapigano hayo yaliyoanza tangu Jumatano ya wiki jana, na kwamba tayari Wakongomani 6,000 wamelazimika kurejea Kongo DR kutokana na ghasia hizo.
Nchi mbili hizo jirani za Kiafrika zimekuwa katika mgogoro kwa muda sasa haswa katika maeneo ya mipakani.
Mwishoni mwa mwaka jana, serikali ya Angola iliwafukuza nchini humo maelfu ya wahamiaji haramu raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ikisisitiza kuwa waliingia nchini humo kinyume cha sheria kwa ajili ya kutafuta madini hususan ya almasi katika mikoa ya Lunda Norte na Lunda Sul.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa hivi karibuni ulitangaza kuwa, mapigano makali kati ya askari wa serikali ya Kongo DR na wanamgambo wa kundi moja la kikabila katika mkoa wa Kasai ndiyo yamewalazimisha watu zaidi ya milioni moja kuyaacha makazi yao na kwenda kuomba hifadhi katika nchi jirani hasa Angola.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇