Rais wa Ethiopia, Mulatu Teshome amesema nchi hiyo karibuni hivi itaanza kuwapa raia wote wa bara Afrika viza mara tu watakapowasili katika nchi hiyo.
Akiongea katika ufunguzi wa bunge la nchi hiyo jana Jumatatu, Rais Teshome amesema nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambayo imekuwa ikitazamwa kama mji mkuu kisiasa wa bara hilo, itaanza kuwapa wananchi wa nchi zote za Afrika viza, mara tu watakapowasili nchini humo, na wala hawatalazimika kutuma maombi ya cheti hicho muhimu cha kusafiria kabla ya safari.
Umoja wa Afrika umewahi kupendekeza kuwa, kuondolewa sharti la viza miongoni mwa wananchi wa bara Afrika ili kuzuru nchi za bara hilo, kutapunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wananchi wa nchi za Kiafrika wanaoligura bara lao kwenda barani Ulaya kutafuta maisha bora.
AU inazitaka nchi za bara hilo kuiga mfano wa serikali za Rwanda na Mauritius, ambazo zimepiga hatua katika uga wa uchumi na uwekezaji kwa kuruhusu wananchi wa nchi nyingine za Afrika kuzuru nchi zao bila viza.
Ushelisheli inatajwa kuwa nchi pekee katika historia, inayowaruhusu wananchi wa Afrika na kutoka maeneo mengine yote ya dunia kuvizuru visiwa hivyo bila viza.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, kila mwaka maelfu ya Waafrika hufa maji katika Bahari ya Meditarenia, wakijaribu kusafiri barani Uropa kupitia Libya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇