Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema( katikati) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Vyoo bora 12 na vyumba Viwili kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule ya msingi Pugu Kajiungeni jijini Dar es Salaa, Wengine kwenye picha ni mwenyekiti wa Hassan Maajar Trust (TMT) Balozi Mwanaidi Sinare Maajar (wapili kulia) Mkuu wa shule ya msingi Pugu Kajiungeni,Ropiana Alponce (Kushoto) pamoja na viongozi wengine, Msaada huo umejengwa na Taasisi ya Hassan Maajar Trust.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema akihutubia wageni waalika katika hafla hiyo.
Wanafunzi wasichana wakipokea baadhi ya zawadi zilizotolewa na marafiki wa taasisi ya HMT wakati wa hafla hiyo.
Mgeni rasmi akikagua miundombinu ya choo cha kisasa kilichojengwa na HMT chini ya mpango wake wa Vyoo Bora kwa Kila shule
---
Taasisi ya Hassan Maajar Trust (HMT), imeendeleza dhamira yake ya kuboresha mazingira ya shule za msingi nchini, ambapo imekabidhi jengo la vyoo shule ya msingi Pugu Kajiungeni, wilaya ya Ilala, Dar es Salaam. Jengo hilo lililogharimu jumla ya Shillingi milioni 65,000.00 lina vyumba 12 na sehemu maalumu kwa wavulana -urinals, ambapo vyumba 2 ni kwa ajili ya ya watoto wenye ulemavu na chumba cha staha kimoja (Dignity Room) kwa ajili ya wasichana wenye mahitaji ya staha.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Hassan Maajar, Balozi Mwanaidi Maajar, alikabidhi vyoo hivyo kwa Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Bi. Rophina Aloyce Kawishe, katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema, ambaye alikuwa mgeni rasmi, walimu, wanafunzi, na wawakilishi kutoka Shirika la Water Aid.
Akiongea katika hafla hiyo, Balozi Maajar amesema “Hii ni mara ya kwanza kwa HMT kujenga vyoo vya shule, na tumefurahia kukamilisha mradi huu wa kwanza.
Kwa kipindi kirefu nyuma, HMT ilikuwa inajulikana kwa kampeni yake kubwa ya ‘Dawati Kwa Kila Mtoto’ ambayo imefanikiwa kwa kutoa madawati 10,000, na kunufaisha zaidi ya wanafunzi 30,000 katika mikoa 13 nchini.
Tuliona vilevile vile kuna changamoto ya uhaba wa vyoo mashuleni. Imekuwa fursa nyingine ya Taasisi ya HMT na wafadhili wake kuunga nguvu kwa pamoja kwa kampeni mpya yenye kauli mbiu, Vyoo Bora Kila Shule.
Aidha amesema, kila safari ni hatua ya kwanza na kwa mradi huu ndiyo hatua ya kwanza kwa HMT kutimiza lengo la kujenga vyoo shule za msingi zilizo na mahitaji na hasa shule zilizo na idadi kubwa ya wanafunzi wenye ulemavu.
Alisema Kupitia hafla tofauti za ukusanyaji fedha kama vile ‘Fundraising Gala’ na ‘Matembezi ya Hiyari’, HMT kupitia kampeni ya Dawati kwa kila Mtoto ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuhamasisha umma kuona kuwa wajibu wa kuboresha mazingira ya shule zetu si wa serikali pekee na kuweza kuchangia madawati hadi pale serikali ilipolivalia njuga tatizo lile.
Kwa HMT ni faraja kubwa kuona idadi kubwa ya watoto wetu siku hizi wakiwa hawakai tena chini.
Kwa kampeni mpya, Vyoo Bora Kila Shule HMT inakusudia kuwasha tena mshumaa kuangazia tatizo la vyoo kwa kuhamasisha umma kuchangia ujenzi wa vyoo katika shule za msingi zilizo na wanafunzi wengi na vyoo vichache.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Sophia Mjema, aliipongeza, HMT, kwa kuamua kuzikabili changamoto za kuboresha mazingira ya elimu kwa kutoa misaada ya madawati, huduma za maktaba na kujenga miundombinu ya vyoo. “Kwa niaba ya serikali nawapongeza kwa jitihada mnazofanya kuboresha mazingira ya kupata elimu mashuleni” alisema.
Taasis ya WaterAid wameisaidia shule kwa kuipa vifaa vya kuvunia maji ya mvua, jambo ambalo limeongeza ubora wa vyoo vilivyojengwa na HMT kwa sababu mazingira ya vyoo yatakuwa masafi naya afya zaidi.
Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi ya Pugu Kajiungeni, Bi. Rophina Aloyce Kawishe, ameishukuru taasisi ya HMT kwa kutoa msaada huo ambao alisema utawezesha wanafunzi wa shule hiyo kusomea katika mazingira rafiki kutokana na kuwa na miundombinu bora ya vyoo na madarasa “Ukosefu wa vyoo vya kutosha kwa muda mrefu imekuwa ni changamoto kubwa katika shule zetu, tunawashukru kwa msaada huu”, alisema.
Taasisi ya Hassan Maajar inafanya maandalizi ya kujenga majengo mengine mawili ya vyoo shule za msingi Nia Njema na Majengo zilizoko Bagamoyo, mkoa wa Pwani. Ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi huu wa kumi na HMT imetenga kiasi cha Shillingi 140 Milioni kwa ajili ya ujenzi huo.
Taasisi ya HMT inajulikana zaidi kwa kampeni yake ya Dawati kwa Kila Mtoto ikiwa ni makakti wa kutimiza ndoto yake ya kuboresha mazingira ya kusomea katika shule za msingi nchini.
Tangu kuanzishwa kwake, imekuwa ikihamasisha umma na kuchangia madawati, kuboresha maktaba na kutoa vitabu, na hasa kwa watoto wa madarasa ya awali ili kujenga tabia ya kujisomea, vile vile kuongeza ufahamu juu ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wakiwa shuleni.
HMT inajivunia mafanikio kwa kuona hamasa kwa watu binafsi, mashirika ya umma na hadi serikali kuamua kulivalia njuga tatizo al upungufu wa madawati shuleni.
Kwa kampeni hii mpya Vyoo Bora Kila Shule, HMT ina imani watu wengi wataendelea kuhamasika kushiriki kwa kutambua kuwa ni jukukumu letu sote kuondoa tatizo la vyoo mashuleni na siyo tu kazi ya serikali peke yake.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇