LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 2, 2018

DK. MNDOLWA: TUTATUMIA SHULE ZETU ZA JUMUIYA YA WAZAZI KUKABILI JANGA LA MMOMONYOKO WA MAADILI

Na Bashir Nkoromo
"Binafsi na kwa nafasi yangu ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), siridhiki na kiwango cha hali ya maadili ndani ya Chama hasa katika ngazi za mikoa, wilaya na kata.

Hii ni kwa kuwa bado wapo baadhi ya wanachama ambao wamekuwa wakifanya matendo kwa wazi au kwa siri kukihujumu Chama katika mambo mbalimbali jambo linaloonyesha dhahiri kwamba linasabishwa na wanachama hao kutokuwa na nidhamu ya kuzingatia maadili ya Chama", anasema Dk. Edmund Mndolwa alipozungumza na mwandishi wa makala hii, hivi karibuni.

Anasema, hali ya kiwango cha baadhi ya wanachama wa CCM kufanya vitendo vya ukiukaji maadili inasababishwa na tabia ya kuoneana haya waliyonayo baadhi ya viongozi waliopewa jukumu la kusimamia maadili ndani ya Chama, jambo ambalo anasema chanzo chake ni rushwa au kulipa fadhila mbalimbali.

" Zipo  kamati za kusimamia maadili katika ngazi mbalimbali lakini pamoja na kuwepo kamati hizo bado mambo hayasimamiwi ipaswavyo, Kama kamati hizi zingekuwa zinafanyakazi zake vizuri, nina uhakika hali ya maadhili ndani ya chama ingetamalaki vya kutosha na kuonyesha tija iliyokusudiwa lakini sasa usimamizi huu unaonekana kufanyika kwa kiwango chake katika ngazi ya taifa tu, huku katika ngazi za mikoa, Wilaya na Kata hali ikiwa kizungumkuti.

Inashangaza sana kuona kwamba Chama kinatoa maelekezo fulani, nfano kumuunga mkono mgombea aliyeteuliwa na Chama, lakini anatokea mwana CCM haungi mkono kwa dhahiri kabisa au kwa siri na hachukuliwi hatua na kamati husika licha ya kwamba kamati hizo zinakuwa zinao ushahidi wa kutosha kwa kila hatua", anasema Dk. Mndolwa.

Dk. Mndolwa anasema, kama tabia ya kuoneana haya inayofanywa na baadhi ya viongozi wa Kamati za maadili ingeachwa kamati hizo zingekuwa mhimili muhimu sana katika kuboresha maadili na nidhamu ndani ya chama kwa kuwa kamati hizo ndizo zenye jukumu hilo kubwa na muhimu kwa Chama kwa kuwa chama ambacho wanachama wake hawafuati maadili kinakuwa hatarini kubakia kuiwa kundi tu jambo ambalo haliwezi kukubalika ndani ya CCM.

Anasema, moja ya faida kubwa ya utekelezwaji wa maadili ndani ya chama ni kwamba hata ufanyajikazi wa serikali katika  kutekeleza ilani ya Chama unakuwa wa hali ya juu katika maeneo yote hasa ya ngazi za chini kwa sababu ufuatiliaji na usimamizi wa utekelezaji wa Ilani hii utafanywa kwa kiwango cha kutosha na viongozi wa CCM.

"Sote ni mashahidi na tunajua Mwenyekiti wetu wa CCM, Rais Dk. John Magufuli hili jambo la maadili ndani ya Chama kwenye nyanja zote amekuwa akilisisitiza na kulisimamia sana ikiwemo pia serikalini, lakini kazi hii hawezi kuifanikisha peke yake kwa sababu nchi ni kubwa na maeneo yanayohitaji usimamizi ni mengi hivyo ni lazima viongozi tumuunge mkono kwa dhati katika suala hilo na pia wanachama na wananchi kwa jumla nao waonyeshe dhamira ya dhati kupokea na kutekeleza maelekezo au maagizo" anasema Dk. Mndolwa.

Anasema, kwa upande wa Jumuiya wa Wazazi Tanzania, yeye na viongozi wenzake wameshakubaliana kuhakikisha wanasimamia kwa vitendo maadili na nidhamu ya chama ndani ya Jumuiya hiyo na kwamba tayari matunda yameanza kuonekana katika maeo mengi.

"Hatusemi tumekwisafanikisha na kuimalia kazi hii, lakini tumefikia pazuri na sisi kama viongozi tunachofanya ni kuongeza  bidii kwa weledi na kuhakikisha tunafika pale inapotakiwa tuwe au chama kiwe kimaadili", anasema Dk. Mndolwa.

WANAOHAMIA CCM
"Ndiyo, jambo hili limeleta mjadala kidogo ndani na nje ya Chama Cha Mapinduzi, lakini kwa kweli hali hii ya Wanachama wa upinzani hasa Wabunge na madiwani kuhamia CCM ina tija kubwa, kwa kuwa moja ya malengo ya Chama chochote ni kuwa na wanachama wengi kadiri inavyowezekana, ili kuwa na nguvu imara ya kukikwezesha Chama kushinda uchaguzi wowote hadi ule wa kukikwezesha kushika dola.

Baadhi wanasema kwamba  Chama kinafanya makosa kwa wanaohamia kuwapa nafasi za kugombea Ubunge au Udiwani, kwamba eti hawaijui ilani ya CCM, si kweli, hawa watu wanaijua ilani ya CCM tena kwa undani sana kwa sababu hata wanapokuwa wangali kwenye upinzani huitumia hiyo hiyo ilani kuipinga CCM.

Tena mimi nionavyo hawa wanaohamia  kwetu wanajua Ilani ya CCM pengine kuliko wanachama wetu wengi, na hili sifanyi mzaha, wewe tafuta mwanachama mmoja tu halafu muulize, ilani inasemaje kuhusu elimu, hatakuambia kitu, kwa hiyo hoja hiyo siyo ya msingi iachwe", anasema Dk. Mndolwa.

Anasema kimsingi wanaohamia CCM ni wale ambao upinzani wao dhidi ya CCM ulikuwa kwa maslahi ya Watanzania na si kwa maslahi yao binafsi na wamehamia baada ya kuridhika kwamba sasa CCM inatekeleza kwa vitendo yale matakwa waliyokuwa wakiyapigania kupitia kambi za upinzani.

USHIRIKI WA JUMUIYA YA WAZAZI KATIKA KAMPENI ZA CCM ZA UCHAGUZI
"Jumuiya zote za Chama tukiwemo sisi wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania, moja ya malengo yake makubwa ni kuhakikisha Jumuiya husika inakuwa mstari wa mbele kukipigania chama kinapokuwa  katika mapambano yoyote.

Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana kila CCM inapoingia katika mapambanano ya Uchaguzi na sisi Jumuiya ya Wazazi tumekuwa tukijipanga kuhakikisha tupo bega kwa bega au mstari wa mbele kusaka kura kwa njia mbalimbali ikiwemo ya mikutano ya kampeni", anasema Dk. Mdolwa akifafanua kuhusu Jumuiya ya Wazazi ambavyo imekuwa ikishiriki katika kampeni za uchaguzi, ukiwemo uchaguzi uliofanyika kwa nyakati tofauti katika majimbo na kata kadhaa, hivi karibuni.

"Kila uchaguzi unapotangazwa, sisi tumekuwa tukijipanga tangu katika ngazi ya taifa, mikoa hadi wilaya, sisi wa ngazi ya taifa japo huwa hatuwezi kwenda viongozi wote kutokana na hali ya kifedha katika Jumuiya yetu, lakini angalau mimi, Makamu wangu na Katibu Mkuu hujipanga na kwenda katika maeneo husika kwa ajili ya kuhamasisha viongozi wetu wa Jumuiya huko, lakini na sisi pia hushiriki mikutano ya ndani na ya hadhara majukwaani kuombea kura wagombea wa Chama chetu", anasema Dk. Mndolwa.

Anasema, Jumuiya ya Wazazi Tanzania, inajiona kuwa inalo jukumu la kuwa mstari wa mbele kuipigania CCM katika kutafuta kura kwa sababu ndiyo Jumuiya ambayo inayo makundi ya jinsia na rika zote ukiacha Chipukizi,  tofauti na Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM) ambayo pamoja na kuwa na jinsia zote lakini ni vijana tu, na Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ambayo wote ni wanawake tu.

"Hatumaanishi kwamba Jumuiya hizi za Wanawake na Vijana hazina umuhimu kwa CCM, la hasha. lakini sisi Jumuiya ya Wazazi tunajivunia kwamba kama mapambano yatahitaji vijana tunao, yakihitaji Wazee tunao au yakihitaji kina mama tu, tunao, kwa hiyo unaweza kuona jinsi ambavyo sisi ni jeshi kubwa kiasi kwamba hatupaswi kuwa nyuma Chama kinapokuwa katika mapambano hasa ya kusaka ushindi kwa njia ya kura", anasema Dk. Mndolwa.

KWA NINI WAPINZANI HUANGUKA KATIKA UCHAGUZI
"Kama unavyojua hakuna kiongozi wa upinzani ambaye hakutokea CCM, wengi kama siyo wote wametoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi. Wanapohama kutoka CCM huondoka na mbinu na aina ya mikakati yetu ambayo hutufanya kushinda uchaguzi, lakini sasa, kwa kuwa CCM ni chama makini kila mara tumekuwa tukipanga mbinu na mikakati kutokana na mahitaji ya wakati uliopo kwa hiyo wanapofika huko na kujaribu kutumia mbinu na mikakati kama yetu hukuta sisi tumeshaibadilisha au kuiboresha na hivyo kuwa na uwezo mkubwa wa kushinda uchaguzi.

Lakini pia CCM inao weledi na ujuzi mkubwa katika masuala ya uchaguzi tofauti na wapinzani, tena CCM inao mfumo mzuri wa kuteua wagombea na kazi hiyo huifanya kwa makini sana kuhakikisha inapitisha wagombea wenye sifa na wanaokubalika ndani na nje ya Chama, tofauti na vyama vya upinzani ambavyo ukitokea uchaguzi humuacha mwanachama wao yeyote mwenye munkari wa kugombea agombee.

Mara nyingi inaonekana kuwa hufanya hivyo bila kumtathmini aliyeomba kugombea kwa tiketi ya chama chao kama anazo sifa za kugombea na anakubalika ndani ya chama chao na kwa wananchi, ndiyo sababu kila uchaguzi unapotokea CCM imekuwa ikiibuka na ushindi mkubwa wa kura au kwa wagombea kupita bila kupigwa kama tulivyoshuhudia katika uchaguzi uliopita hivi karibuni katika majimbo na kata kadhaa ambapo CCM imeshinda kwa kishindo kwa kura na kupita bila kupingwa huku wapinzani wakibakia kudai kuwa CCM imefanya hila au kuiba kura.

Baadhi ya uchaguzi ambao hali hiyo imetokea no ule wa Buyungu mkoani Kigoma, Monduli mkoani Arusha, Korogwe Vijijini mkoani Tanga na Ukonga jijini Dar es Salaam na Kata nyingi tu.

Si hivyo tu, Wananchi sasa wana imani na CCM kuliko ilivyokuwa nyuma, hali ya utekelezaji wa ilani ya CCM inayofanywa na serikali chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli imevutia na kuwatia imani Wananchi wengi sana, jambo ambalo sasa siyo jambo la kushangaza CCM inapoingia katika uchaguzi na kuibuka na ushindi wa kishindo kwa kura au kupita bila kupingwa", anasema Dk. Mndolwa.

Kuhusu wanachama wa upinzani hasa wabunge na madiwani kuhamia CCM, Dk. Mndolwa anasema jambo hilo lina tija sana kwa CCM kwa kuwa lengo la chama chochote cha siasa ni kuwa na wanachama wengi kadri inavyowezekana ili kiweze kushinda katika uchaguzi mbalimbali hasa ule wa kukifanya kishike dola, hivyo wanaobeza wanapotoka kwa sababu hawaelewi au wanazo sababu zao binafsi.

"Tena hawa wanaohamia CCM ni watu muhimu sana kwa sababu wanahama vyama vyao kwa sababu ya maslahi ya wananchi na si kwa maslahi yao binafsi. ukiwatazama hawa utagundua kuwa wao walikuwa wapinzani kwa maslahi ya Watanzania na si kwa maslahi yao, hii ni kwa sababu wengi wao wanahama kutokana na kuridhika kwamba yale yaliyokuwa yakiyadai sasa yanatekelezwa na CCM tena kwa kiwango kinachozidi madai yao.

Wameshuhudia kuwa sasa nchi chini ya Uongozi wa Rais Dk. Magufuli imeimarisha mapambano dhidi ya umangimeza na utumiaji wa hovyo wa rasilimali na mapato ya nchi, huduma mbalimbali zimeanza kuimarika hasa katika sekta za elimu, afya, usafiri na usafirishaji na miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali nchini", anasema Dk. Mndolwa.

Kuhusu baadhi ya watu wakiwemo wana CCM wanaodai kwamba, CCM inakosea kuwapa nafasi za kugombea wale wanaohamia CCM kwa madai kwamba ni wageni na pia hawajui vema ilani ya CCM Dk. Mndolwa anasema madai hayo siyo sahihi.

"Kwanza nataka ujue kwamba CCM huwateua kugombea kulingana na maelekezo ya Katiba ya CCM ambayo inaipa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya taifa ya CCM, mamlaka ya kuteua wagombea, na hili la kwamba ni wageni, si kweli wengi wao wamewahi kuwa wana CCM waandamizi lakini kutokana na sababu mbalimbali wakahama CCM, sasa kurejea kwao CCM hakuwafanyi kuwa wageni wasiojulikana kabisa, ila cha msingi tukiwa nao lazima kujiridhisha kuwa wamerejea kwa dhati kweli ya mioyo yao.

Lakini kuhusu Ilani ya CCM, mimi naamini hawa wanaijua sana, na ninadhani wanaweza kuwa wanaijua kuliko hata baadhi ya wana CCM wetu wengi, kwa kuwa upo ushahidi kwamba huwa wanaisoma sana ilani ya CCM na ndiyo maana wakiwa upinzani hupitia ndani ya ilani hiyo kutafuta hoja za kuipinga CCM, lakini hata wanapohamia CCM wakipewa kugombea huwa majukwaani wanaviainisha vifungu mbalimbali vya ilani wakati wakitoa ahadi ya kuwatumikia wananchi watakapochaguliwa.

JUKUMU LA MMOMONYOKO WA MAADILI
"Jambo hili la kupambana na mmomonyoko wa maadili tulilipokea likiwa ni agizo la Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Magufuli alilolitoa kwentu wakati wa Mkutano Mkuu wa tisa wa Jumuiya ya Wazazi uliofanyika mjini Dodoma, Desemba 12, 2017, ambako Jumuiya hii ya Wazazi ilikuwa katika uchaguzi wa kupata safu mpya ya uongozi ngazi ya taifa.

Hapa shaka jukumu hili tutalifanya tena kwa weledi mkubwa, tayari tumeshaanza kutafakari jinsi tutakavyoweza kufanikisha kama Jumuiya  na ninadhani tutaliweza kwa kuwa licha ya kuagizwa na Mwenyekiti wetu, lakini pia ni moja ya jukumu letu kama wazazi", anasema Dk. Mndolwa.

Anasema, pamoja na athari kubwa katika mmomonyoko wa maadili kuchangiwa na utandawazi, lakini bado wazazi wapo katika nafasi ya kulaumiwa kwa kuwa inaonyesha wazi kuwa wengi wao sasa wamejikita tu katika shunghuli za kila siku za kukimu maisha yao na kusahau kabisa suala la malezi ya watoto wao kama vile siyo jukumu lao.

"Binti anatoka nyumbani kwao amevaa mavazi yayoonyesha sehemu ya matiti yake au nguo zinazobana na kuonyesha ramani nzima ya maungo yake, lakini  baba na mama au mlezi wake hawamkemei, wanatazama kama jambo la kawaida, au mtoto wa kiume anatoka nyumbani amevaa 'mlegezo' suruali au kampula na kusababisha mwendo wake kuwa wa ajabu, lakini baba na mama yake au mlezi hawamkemei", anasema Dk. Mndolwa.

Anasema pia tabia ya baadhi ya wazazi kudekeza watoto inachangia watoto kutumbukia katika mmomonyoko wa maadili kwa sababu inamfanya mtoto kujipangia na kuamua kufanya anavyotaka wakati umri wake haumruhusu.

" Unakuta mzazi anampa fedha nyingi mtoto wakati wa kwenda shule, halafu akiulizwa anasema "mimi nilisoma kwa taabu sitaki mtoto wangu naye asome kwa taabu", akidhani kumpatia fedha nyingi ndiyo anamfanya mtoto asome kwa raha kumbe anamsababishia kuharibikiwa, maana kitendo cha mtoto kuwa na fedha nyingi kitasababisha mtoto kutumbukia katika anasa na makundi ya watoto wabaya ambao watamshawishi kuwa nao ili wazitumie fedha zake.

Baada ya kutumbukia katika makundi mabaya mtoto atakuwa akipenda starehe na anasa na kusahau kabisa masomo au kuwa na uelewa mdogo kimasomo na hatimaye anatumbukia katika kutumia dawa za kulevya au uvutaji bangi au vyote pamoja", anasema Dk. Mndolwa.

Anasema, mazoea ya kuwa na fedha nyingi, pia yanaweza kusababisha mtoto wa kiume kuwa mwizi, kibaka au hata jambazi ili kusaka fedha pale anapokuwa ameishiwa alizopewa na mzazi, huku kwa upende wa mtoto wa kike akitumbukia katika kupata mimba za  utotoni au kabla ya kumaliza msomo kwa sababu ya kujiingiza katika mambo ya ukahaba kutafuta fedha anapoishiwa zile alizopewa na mzazi.

"Sasa ili kukabiliana kwa vitendo na suala hili la mmomonyoko wa maadili tumepanga kuliasisi kwa nafasi kubwa katika shule zetu ambazo tunamiliki katika mikoa kadhaa hapa nchini, tutahakikisha baada ya kuziboresha shule zetu 55 zinakuwa na mafunzo maalum kuhusiana na maadili na tutaelekeza walimu kwenye shule zetu kuwa wafuatiliaji na wakali zaidi katika jambo hili. Pia tutaweka programu za kutoa mafunzo kwa wanafunzi  kupitia njia mbalimbali ikiwemo wataalam wa saikolojia", anasema Dk. Mndolwa.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages