Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza wamezungumza kwa nyakati tofauti na Mfalme Salman bin Abdulaziz Al Saud wa Saudia kuhusiana na faili la kuuawa Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari na mkosoajia wa utawala wa Aal-Saud.
Ikulu ya Élysée nchini Ufaransa imetangaza kwamba katika mazungumzo hayo ya simu, Rais Macron amesisitiza kwamba Paris kwa kushirikiana na washirika wake itachukua hatua ya kuwawekea vikwazo wahusika wa mauaji ya Khashoggi. Sambamba na kuonyesha kuchukizwa na mauaji dhidi ya mwandishi huyo wa habari, Rais Emmanuel Macron ametaka kuwekwa wazi masuala yote yanayohusiana na mauaji ya Jamal Khashoggi. Kwa upande wake Theresa Mary May, Waziri Mkuu wa Uingereza amemtaka Mfalme Salman kutoa majibu ya kuridhisha kuhusiana na mauaji ya mwandishi huyo. Katika mazungumzo yake ya simu na mfalme huyo wa Saudia, May amesema kuwa maelezo ya Saudia kuhusiana na kuuawa Khashoggi ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul, Uturuki, hayaingii akilini na kwamba ni lazima liwekwe wazi haraka tukio zima la mauaji hayo.
Kadhalika Waziri Mkuu huyo wa Uingereza ameitaka serikali ya Saudia kushirikiana na serikali ya Uturuki katika uchunguzi na kutangazwa matokeo ya uchunguzi huo. Ameongeza kwamba Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza imeshawazuia watuhumiwa wote wa mauaji ya Khashoggi kuingia nchi hiyo na kwamba iwapo watu hao walikuwa wameshapatiwa vibali vya kuingia Uingereza, basi vibali hivyo vitabatilishwa. Awali mwendesha Mashtaka Mkuu wa Saudia alidai kwamba ugomvi wa kimaneno uliojiri kati ya Khashoggi na maafisa wa usalama wa Saudia ndani ya ubalozi mdogo wa nchi hiyo mjini Istanbul, ndio uliozua mapigano yaliyosababisha mwandishi huyo kupoteza maisha. Hata hivyo taarifa hiyo imekabiliwa na radiamali kali duniani, ambapo nchi nyingi zimesema kuwa maelezo ya Saudia yanapingana na taarifa ya awali ya Riyadh kwamba mwandishi huyo aliondoka katika jengo la ubalozi huo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇