Shughuli za ufunguzi wa mazungumzo ya amani ya Burundi zilizokuwa zifanyike jana Jumatano mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania zililazimika kusogezwa mbele ingawa msimamizi wa mazungumzo hayo Rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mkapa hakueleza sababu.
Hata hivyo taarifa za ndani zimedai kuwa msimamizi wa mazungumzo hayo ametuma ujumbe wake kwa serikali ya Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi akiitaka wawakilishi katika mazungumzo hayo.
Awali serikali ya Burundi ilisema haitaweza kushiriki katika mazungumzo hayo kwa kuwa nchi hiyo iko katika maombolezo ya mwezi mzima kuwakumbuka mashujaa wa taifa hilo kwa mujibu wa Evariste Ndayishimiye Katibu Mkuu wa chama tawala cha CNDD-FD.
Duru nyingine zinasema kuwa, serikali ya Bujumbura imetaka mazungumzo hayo yasogezwe mbele.
Mazungumzo hayo ambayo yalitarajiwa kuanza jana na kuendelea hadi tarehe mwezi huu yalitarajiwa kujikita katika kusaka muafaka kuhusu namna bora itakayosadia pande hizo kushiriki kwa uhuru na uwazi katika maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Wajumbe wa upinzani waishio nje ya Burundi wanaojumuika katika Muungano wa CNARED pamoja na wajumbe wa upinzani wa ndani wa muungano wa AMIZERO YA BARUNDI” unaoongozwa na Agathon Rwassa wapo Arusha tayari kwa mazungumzo hayo.
Tangu mazungumzo ya amani ya Burundi yaanze Disemba 2015 hadi sasa hakujapigwa hatua yoyote ya maana, na wapinzani wanaituhumu serikali ya Bujumbura kwamba, haina nia ya dhati ya kuhakikisha mazungumzo hayo yanakuwa na natija. Burundi ilitumbukia katika machafuko ya kisiasa mapema mwaka 2015 baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu; hatua ambayo ilitajwa kuwa ni kinyume na katiba ya nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇