Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akipokea cheti cha nafasi ya kwanza ya mtoa huduma za kitaalam kutoka kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Elias Kwandikwa kutokana na Taasisi hiyo kushiriki katika kutoa huduma ya upimaji wa magonjwa ya moyo kwenye mkutano wa wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dorica Burengelo akimpima ugonjwa wa kisukari mhandisi aliyetembelea banda la hiyo kwa ajili ya kupima afya na kupata elimu ya lishe na mazoezi wakati wa mkutano wa 16 wa wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Theophylly Mushi akimpima msukumo wa damu (PB) mhandisi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima afya na kupata elimu ya lishe na mazoezi wakati wa mkutano wa 16 wa wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hussein Mube akimpa ushauri wa kiafya mhandisi aliyetembelea banda la Taasisi hiyo kwa ajili ya kupima afya na kupata elimu ya lishe bora na mazoezi wakati wa mkutano wa 16 wa wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam
Washiriki wa upimaji afya, utoaji wa elimu ya lishe bora na mazoezi wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi mara baada ya kupokea cheti cha kushika nafasi ya kwanza ya mtoa huduma za kitaalam kwenye mkutano wa wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiangalia huduma za upimaji wa magonjwa ya moyo kwa wahandisi zilivyokuwa zinatolewa katika banda la Taasisi hiyo wakati wa mkutano wa 16 wa wahandisi uliofanyika kwa siku tatu Jijini Dar es Salaam. (PICHA ZOTE NA JKCI)
Na Mwandishi Maalum
07/09/2018 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeombwa kuwafikia wananchi wengi zaidi wakiwemo wafanyakazi ili waweze kufanyiwa vipimo vya moyo pamoja na kupata elimu ya jinsi ya kuepukana na ugonjwa huo.
Ombi hilo limetolewa leo na washiriki wa mkutano wa mwaka wa wahandisi uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Diamond Jubilee uliopo jijini Dar es Salaam.
Wahandishi hao pia wamewashauri wafanyakazi kutenga muda wa kupima afya zao na kufanya mazoezi ambayo yatawasaidia kiafya.
Mhandisi Alex Kalanje alisema kama Taasisi hiyo itawafikia watu wengi zaidi kwa kwenda katika mikusanyiko mbalimbali kutawasaidia watanzania wakiwemo wafanyakazi ambao kutokana na majukumu yao ya kazi wanakosa muda wa kwenda kupima afya zao kupata huduma ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo.
“Wafanyakazi wengi wanakosa muda wa kwenda Hospitali kupima afya zao, lakini kama kutakuwa na utaratibu wa kuwepo kwa wataalam wa afya katika mikutano mbalimbali kutawasaidia kupata muda wa kupima kirahisi zaidi kuliko wanapokuwa katika maeneo yao ya kazi”, alisema Mhandisi Kalanje.
Kwa upande wake Mhandisi Dkt. Gemma Modu aliwashauri watanzania kutenga muda wa kupima afya zao kwa kufanya hivyo kutawasaidia kujuwa kama wanamatatizo au la na kama wanayo wataweza kupata matibabu mapema.
Aidha Dkt. Gema pia aliwasihi kinamama kubadilika na kuhamasisha familia zao kwenda kupima na ikifika muda wa kupima waende wao na waume zao pamoja na watoto.
Akizungumza wakati wa kufungwa kwa mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dkt. Jim James Yonazi aliipongeza Taasisi ya Moyo kwa huduma ya kijamii iliyoitoa ya upimaji na kutoa elimu ya lishe pamoja na mazoezi na kusema kuwa kazi waliyoifanya ni kubwa.
Taasisi hiyo ilishika nafasi ya kwanza ya mtoa huduma za kitaalam kwa kutoa huduma za upimaji wa vihatarishi vya magonjwa ya Moyo, ushauri wa kiafya kuhusiana na Magonjwa ya Moyo, elimu ya lishe bora na mazoezi, kueleza kwa kina huduma zinazotolewa na Taasisi, kutoa dawa bure kwa watu waliokutwa na matatizo ya moyo na kutoa rufaa ya moja kwa moja kwa wagonjwa waliokutwa na matatizo ya moyo yaliyohitajika kupewa rufaa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇