Makamu wa Rais, Samia Hassan Suluhu ameagiza kukamatwa mara moja baadhi ya watu wanaotumia jina lake na kuwadanganya wananchi kwa kuwachangisha fedha ili wapate Sh50 milioni zilizoahidiwa katika kampeni za uchaguzi Mkuu 2015.
Kauli hiyo imekuja siku moja mara baada ya makamu huyo wa Rais kusema fedha hizo zitatumika katika miradi mbalimbali ya maendeleo na sio kupewa wananchi moja kwa moja kama walivyoahidi awali.
Ameyabainisha hayo leo Septemba 11, wakati akizungumza na wananchi, viwanja vya Soweto katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Munzeze wilayani hapa mkoani Kigoma mara baada ya kumaliza kuzindua zoezi la kupanda miti.
"Kuna wanjanja wanapita katika vijijini wakitumia jina langu na kuwadanganya wananchi huku wakiwachangisha fedha kuwaambia watakaowahi kutoa watakuwa wakwanza kupata Sh. 50 Milioni zilizotengwa, huu ni uongo na hao ni matapeli wakamatwe mara moja,"amesema Mama Samia.
Amesema kuna baadhi ya watu wamekuwa wakipita vijijini na kuwachangisha fedha ili wapate Sh50milioni na kuwaambia wametumwa na makamu wa Rais jambo ambalo si kweli lazima watu hao wachukuliwe hatua mara moja.
Amesema fedha iliyopo serikali kwa sasa yote ni ya kufanya maendeleo kwa wananchi na kuwaasa wananchi waepuke matapeli.
“Mtu yeyote anayekuja kwenu na kukusanya fedha kwa ajili hiyo mkamateni na muitieni polisi mara moja hii pesa bado kutoka, kwasasa tunashugulikia mambo mengine," amesema Makamu wa Rais.
Awali akizungumza katika mkutano huo Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wazazi kushirikiana na serikali kwa kutokomeza utoro mashuleni kwa kuwahimiza watoto wao kwenda shule.
Amesema kwa sasa serikali inatumia kiasi kikubwa cha fedha katika kuwekeza kwenye sekta ya elimu ambapo kila mwezi inatoa zaidi ya Sh20 bilioni.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa zoezi la upandaji miti, Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu wilaya ya Buhigwe(TFS), William Samweli amesema changamoto iliyopo wilayani hapo ni ukosefu wa ardhi ya kutosha kupanda miti.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇