Watu 43 wamepoteza maisha huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya basi la abiria kubingirika kwenye bonde, katika wilaya ya Jagtial kusini mwa India.
Duru za habari zimeripoti kwamba, basi hilo lilikuwa limebeba abiria 55 waliokuwa wametoka hekaluni katika matambiko ya kidini, katika eneo la milima lililoko kwenye jimbo la Telangana kusini mwa nchi mapema leo, kabla ya kupoteza muelekeo na kubingirika bondeni.
Mashuhuda wanasema dereva wa basi hilo lililokuwa likitokea eneo la hekalu la Anjaneya Swamy katika wilaya ya Jagtial alipoteza muelekeo alipojaribu kukwepa kugongana ana kwa ana na basi jingine katika eneo hilo lenye shughuli nyingi.
Baadhi ya majeruhi hata hivyo wanasema dereva huyo alikuwa akiliendesha basi hilo kwa mwendo wa kasi ndipo akapoteza muelekeo.
Itakumbukwa kuwa, watu 33 waliaga dunia katika ajali nyingine mbaya ya barabarani iliyotokea mnamo Juni 28, baada ya basi lililokuwa limebeba wafanyakazi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Dapoli kubingiria bondeni katika jimbo la Maharashtra, magharibi mwa nchi, siku chache baada ya watu wengine 48 kupoteza maisha katika ajali nyingine iliyotokea chini ya milima ya Himalaya.
Zaidi ya watu 150,000 huaga dunia kila mwaka nchini India katika visa mbalimbali vya ajali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇