Jean Pierre Bemba, Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametanagaza kuwa, atamuuunga mkono mgombea wa upinzani katika uchaguzi ujao wa rais.
Jean Pierre Bemba ambaye amezuiwa na Tume ya Uchaguzi ya DRC (CENI) kugombea urais kwa msingi kuwa alipatikana na hatia katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, amesema kuwa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo bado iko mbali mno katika kufikia viwango vya uchaguzi wa kidemokrasia.
Amesisitiza kuwa, kama uchaguzi ujao wa DRC utafanyika katika mazingira ya kidemokrasia na endapo wapinzani wataungana na kusimamisha mgombea mmoja katika kiti cha urais, basi atamuunga mkono mgombea huyo na kumfanya aibuke na ushindi.
Uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umepangwa kufanyika Desemba 23 mwaka huu. Mbali na chama tawala, vyama vya upinzani nchini humo vimeshatangaza wagombea wao watakaochuana na mgombea wa chama cha Rais Kabila.
Hata hivyo wapinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wameendelea kulalamikia kile wanachokisema kuwa, ni kutokuweko maandalizi ya kutosha ya kufanyika uchaguzi huru na haki huku suala la kuzuiwa baadhi ya wagombea kushiriki katika uchaguzi huo likiendelea kuwa kilio cha wapinzani nchini humo.
Chama tawala cha Rais Joseph Kabila kilimtangaza Emmanuel Ramazani Shadary kuwa mbeba bendera ya chama hicho pamoja na vyama tanzu katika uchaguzi ujao wa mwishoni mwa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇