LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 18, 2018

WAGONJWA 22 WAPATA MATIBABU KATIKA KAMBI MAALUM YA TAASISI YA MOYO YA (JKCI)


Na Genofeva Matemu na Salome Majaliwa
17/08/2018 Jumla ya wagonjwa 22 wenye  matatizo  ya moyo yatokanayo na mfumo wa umeme wa moyo  usiofanya kazi sawasawa wamefanyiwa upasuaji mdogo na  kuwekewa vifaa maalum vitakavyousaidia moyo kufanya kazi vizuri.
Matibabu hayo yamefanyika katika kambi maalum ya siku  saba iliyofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  kwa mgonjwa kufanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa kutumia mtambo wa Cathlab.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa Kurugenzi  ya Magonjwa ya moyo ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Moyo Peter Kisenge alisema kambi hiyo inafanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo kwa kushirikiana na wenzao wa  nchini Marekani kutoka Shirika la  Madaktari Afrika.
Dkt. Kisenge alisema kambi hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo ambao mapigo yao yako chini  kwa asilimia hamsini kwa dakika kwa kuwawekea  kifaa  maalum akinachosaidia mapigo  ya moyo kuongezeka (Pacemaker).
“Kazi ya kifaa hiki  maalum cha mfumo wa umeme wa moyo ni kuwasaidia wagonjwa  wasipoteze maisha ghafla,  kwani mara nyingi wagonjwa wenye matatizo ya mapigo ya  moyo ambayo yako chini hufa vifo vya  ghafla”, alisema Dkt. Kisenge.
Kuhusu matibabu waliyopatiwa wagonjwa katika kambi hiyo Dkt. Kisenge alisema zoezi limeenda vizuri na kwa ufanisi mkubwa kwa wagonjwa  kuwekewa vifaa vya pacemaker na ICD (Implantable cardioverter defibrillator - ICD) kwa wagonjwa ambao mapigo yao ya moyo yako chini ya asilimia 30.
Kwa upande wake Prof. Matthew Sackett kutoka Madaktari Afrika alisema kambi hiyo ilienda   sambamba na utoaji wa elimu kwa madaktari na wataalam wengine wa afya ambao baada ya mafunzo hayo wataweza kuwawekea wagonjwa  kifaa cha ICD ambapo kabla ya hapo hawakuwa wanaweza kufanya hivyo.

“Wiki hii imekuwa ni wiki ya mafanikio kwetu, tumetibu wagonjwa na nimetoa elimu ya namna ya kumuwekea mgonjwa kifaa cha  ICD kwa madaktari na wataalam wengine wa afya,  kila nitakapopata nafasi nitakuja kutoa huduma kwa wagonjwa na elimu kwa wafanyakazi”, alisema Prof. Sacckett.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages