JESHI la Polisi mkoani Morogoro, linawashikilia watuhumiwa tisa kwa tuhuma za wizi wa mafuta ya dizeli lita 570, mali ya kampuni zinazoshughulika na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) zilizopo Ngerengere mkoani hapa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Willibrod Mutafungwa, watuhumiwa hao walikamatwa Julai 17 majira ya jioni saa 10 jioni ilipoanza operesheni maalum ya Jeshi la Polisi na kwamba msako unaendelea mkoani hapa.
Kamanda Mutafungwa alisema, watuhumiwa hao walikamatwa na mafuta hayo yakiwa kwenye madumu ya lita 20 na lita 40 kila moja.
Alisema majina ya watuhumiwa hao yamehifadhiwa kwa ajili ya kuepusha uwezekano wa kuvuruga upelelezi unaoendelea.
Wakati huo huo Anna Selestin (30), mfanyabiashara na mkazi wa Manzese Manispaa ya Morogoro, anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kukamatwa na dawa zinazidhaniwa ni za kulevya aina ya Heroin kete 47 zikiwa kwenye kikopo cheusi.
Kamanda huyo alisema tukio hilo lilitokea Julai 30 majira ya mchana katika eneo la Manzese na kwamba vitu vingine alivyokutwa navyo ni bangi puli 15, kete za bangi 20 na misokoto 160.
Kamanda Mutafungwa aliongeza kuwa uchunguzi zaidi unaendelea, huku taratibu za kumfikisha mahakamani zikiendelea.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇