MKURUGENZI wa Mashtaka (DPP), amekiri kupokea malalamiko kutoka pande zote mbili katika kesi inayomkabili mke wa marehemu Bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake dhidi ya mauaji ya dada wa bilionea huyo, Aneth Msuya.
Aidha, DPP ameeleza kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita akitoa madai hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Mwita alidai kuwa jalada la kesi hiyo lipo mikononi mwa DPP kwa ajili ya utendaji zaidi wa kikazi.
“Mheshimiwa hakimu, DPP amekiri kupokea malalamiko ya pande zote mbili, anaomba mahakama imvumilie wakati analifanyia kazi jalada la kesi hiyo, ili maelekezo atakayotoa yawe ya haki,” alidai Mwita.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alidai kuwa hana pingamizi na hoja za Jamhuri na kwamba DPP apewe muda wa kutosha kutenda haki kwa pande zote mbili.
Hakimu alisema upande wa Jamhuri ufuatilie jalada hilo ili mahakama iweze kuendelea na kesi hiyo, Mbali ya Miriam, mshtakiwa mwingine ni mfanyabiashara, Revocatus Muyela.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuwa Mei 25, 2016 walimuua kwa makusudi dada wa marehemu Bilionea Erasto Msuya, Aneth Msuya.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇