RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar zitaendelea kuimarisha uhusiano wa kidugu na kihisitoria uliopo baina yake na Burundi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha amani ya Burundi inadumu.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Agosti 20, 2018, Ikulu mjini Unguja, Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Balozi wa Burundi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gervais Abayeho aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha.
Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejidhatiti katika kushirikiana na Burundi kwa lengo la kukuza uhusiano na mashirikiano yaliopo sambamba na kuimarisha amani na utulivu.
Dk. Shein alipongeza amani na utulivu iliyopo Burundi pamoja na kueleza juhudi za muda mrefu zilizochukuliwa na viongozi wa Tanzania katika kuhakikisha Burundi inakuwa salama huku akitumia fursa hiyo kupongeza hatua zilizochukuliwa kuipata Katiba mpya ya nchi hiyo.
Alieleza juhudi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuimarisha sekta ya utalii na kueleza haja ya kuwepo mashirikiano katika kuimarisha sekta hiyo huku akieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha sekta ya uvuvi ambayo inaweza kuimarisha sekta ya biashara ya samaki kati ya Zanzibar na Burundi.
Kwa upande wa sekta ya elimu, Dk. Shein alieleza haja ya kuwepo kwa mashirikiano katika sekta hiyo hasa ikizingatiwa kuwa tayari Zanzibar inavyo vyuo vyake Vikuu vitatu ambavyo vinatoa taaluma mbali mbali hivyo ipo haja ya kushirikiana na vyuo Vikuu vya nchi hiyo sambamba na kubadilishana wafadhili kati ya vyuo vikuu hivyo.
Aidha, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchini Burundi kuja kuekeza hapa Zanzibar kutokana na fursa mbali mbali zilizopo huku akimpongeza Rais Nkurunziza kwa kukikuza na kukiendeleza Kiswahili nchini humo.
Pia, Rais Dk. Shein alimuhakikishia kiongozi huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na yeye mwenyewe ataendelea kushirikiana nae katika kuhakikisha anafanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.
Nae Balozi wa Burundi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Gervais Abayeho alipongeza juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Burundi katika kuhakikisha iko salama na wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu mkubwa.
Aidha, Balozi Abayeho alieleza uhusiano na mashirikiano mazuri yaliopo kati ya Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar na nchi ya Burundi.
Balozi Abayeho alitumia fursa hiyo kuipongeza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia uraia wakimbizi wenye asili ya Burundi zaidi ya laki mbili ambao waliishi kwa muda mrefu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇