Mwanafunzi
wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Ibutamisuzi, Kata ya Mbutu
wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, Nchambi Malunde (9), amenusurika kufa
baada ya kujeruhiwa vibaya na fisi wakati akienda shuleni na mwanafunzi
mwenzake.
Mama
wa mwanafunzi huyo, Masaaka Mwandu, alisema tukio hilo lilitokea Ijumaa
majira ya asubuhi wakati mwanaye akiwa na mwanafunzi mwenzake wa darasa
la kwanza ambaye hata hivyo, hakumtaja jina wakiwa njiani kwenda
shuleni ndipo walipovamiwa na fisi.
Alisema
baada ya fisi huyo kuwavamia, alianza kumng'ata mwanae, hivyo kupiga
kelele kuomba msaada, hali iliyomfanya mwanafunzi mwenzake kutimua mbio
kwenda kutoa taarifa kwenye nyumba ya jirani ambapo wananchi walifika
eneo hilo wakiwa na mikuki, mashoka, mapanga na marungu.
Kwa
mujibu wa Mwandu, pamoja na wananchi kufika kwenye eneo la tukio na
kuanza kumfukuza fisi huyo, aliamua kumuachia mwanafunzi na kuwageukia
wananchi akiwatishia kuwashambulia kisha kutoweka na mfuko wa madaftari
ya mwanafunzi huyo.
Mama
huyo alisema baada ya fisi kutoweka, ndipo wananchi walipomchukua
mwanae na kumpeleka nyumbani ili apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Igunga
kwa matibabu, lakini kabla hawajaondoka fisi huyo alifika nyumbani kwa
mwanafunzi huyo huku akiwa na mfuko wa madaftari mdomoni na ndipo
wananchi walimfukuza tena.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Ibutamisuzi, Ludovick Ngassa, alisema baada ya
kumuokoa mwanafunzi huyo waliamua kupiga simu Idara ya Maliasili kuomba
msaada na ndipo maofisa wanyamapori walifika kijijini hapo na kuanza
kumsaka fisi huyo bila mafanikio.
Naye
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi, Ibutamisuzi, Alex Simumba,
alithibitisha kwamba mwanafunzi huyo anasoma katika shule hiyo na
kuiomba Idara ya Maliasili kumsaka fisi huyo hadi apatikane ili kunusuru
maisha ya wanafunzi wengine.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Merchades Magongo,
alithibitisha kumpokea Nchambi akiwa amejeruhiwa vibaya sehemu za
begani, maeneo ya makalio na kusema kuwa amelazwa wodi namba nane na
hali yake si nzuri na kwamba majeraha aliyonayo ni makubwa.
Mkuu
wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Igunga, Jahulula Edward,
alisema baada ya kupewa taarifa na mtendaji wa kijiji hicho juu ya fisi
huyo, walikwenda hadi eneo hilo ambapo kwa kushirikiana na wananchi
walimtafuta bila mafanikio na kuongeza kuwa wanaendelea kumsaka hadi
apatikane.
Kwa
mujibu wa Jahulula, pamoja na kumjeruhi mwanafunzi pia fisi huyo
alimshambulia ndama hadi kufa, na kutoa wito kwa wananchi kutoa taarifa
pindi watakapomuona fisi huyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇