Dar
es Salaam, 17/08/2018. Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) imesaini
mkataba wa ushirikiano na hospitali ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking cha
Beijing nchini China. Mkataba huo utajikita katika maeneo ya tiba, utafifi na
mafunzo.
Mkataba
huo umesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Respicious Boniface pamoja na
Rais wa hospitali ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking Ms Hongxia Yu ambapo
MOI itanufaika katika kuboresha huduma za kibingwa za daraja la juu (Super
specialised services) katika maeneo ya upasuaji wa Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa
ya Fahamu.
Hafla
ya kusaini mkataba huo imeshuhudiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mh Ummy Mwalimu pamoja na Balozi wa Tanzania nchini
China Mh. Balozi Mbelwa Kairuki pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhamad
Kambi.
Aidha,
hatua hiyo imefikiwa baada ya Waziri wa Afya Mh Ummy Mwalimu ambaye yuko kwenye
ziara ya kikazi nchini China kufanya kikao na Rais wa Hospitali ya kimataifa ya
chuo kikuu cha Peking jijini Beijing kuhusiana na kushirikiana na Serikali ya
Tanzania katika kuboresha huduma za tiba za kibingwa hapa nchini.
Hospitali
ya kimataifa ya Chuo Kikuu cha Peking ina uzoefu mkubwa katika matibabu ya
Mifupa, Ubongo, Mgongo na Mishipa ya fahamu ambapo ina vitanda 1800 vya kulaza
wagonjwa, ICU vitanda 171, Vyumba vya upasuaji 48 na kwa mwaka inahudumia zaidi
ya wagonjwa milioni 14.7
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇