Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amewaonya Polisi nchini ambao wanatumiwa na mafisadi kuwanyanyasa wananchi maskini kwa kupora ardhi zao na kukimbilia kufungua kesi vituoni wakilazimisha ardhi hiyo iwe mali yao.
Akizungumza na mamia ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Ragati, Kata ya Kasuguti, Jimbo la Mwibara, wilayani Bunda, Mkoa wa Mara, Lugola alisema amepata malalamiko mengi kutoka sehemu mbalimbali nchini, kuwa mafisadi uonea wananchi maskini kwa kupora kwa nguvu ardhi wakidai wanamiliki wao na wanatumia badhi ya polisi wasiokua waaminifu ili kuwakandamiza wananchi hao.
Kutokana na hatua hiyo, Lugola amepiga marufuku kwa mwananchi yeyote ambaye anakurupuka kukimbilia kituo cha polisi kufungua kesi za ardhi ambazo hazina uthibitisho wa jinai yoyote, badala yake kesi au malalamiko yake kwanza ayapeleke katika mabaraza ya ardhi katika eneo husika ili ziweze kutatuliwa.
Lugola ameongeza kuwa, mafisadi hao ambao wanafedha baada ya kuona mmiliki halali wa ardhi hiyo anagoma kuondoka katika sehemu husika, basi utumia fedha zake kwa kukimbilia polisi kufungua kesi bila ya kuwa na uthitisho wowote huku baadhi ya polisi wasiokua waaminifu wakitumiwa katika kufanikisha ardhi hiyo ananyang’anywa mwananchi huyo.
“Kuanzia leo mwananchi yeyote atakaeenda kufungua kesi kituo cha polisi inayohusu masuala ya ardhi na endapo kiwanja hicho kimepimwa lazima awe na hati inayoonyesha yeye ni mmiliki halali, ili iwasaidie polisi wajue wewe ndio mmiliki halali, na kwa upande wa ardhi ambayo haijapimwa lazima mwananchi huyo aende polisi akiwa na uthibitisho kutoka kijijini au katika mtaa unaosema kwamba eneo hilo ni la kwako na polisi wathibitishe hilo,” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kuwa, na endapo kesi ya mlalamikaji yeyote ipo mahakamani anapaswa kuheshimu makahama na si kuendeleza kufanya usumbufu katika jamii pamoja na kwenda polisi na kuanza kutafuta njia ya kumsumbua mwananchi ambaye ni maskini katika eneo hilo.
Katika hilo, Lugola alifafanua kuwa, endapo mwananchi ana hukumu ya mahakamani inayoonyesha ameshinda kesi hiyo, mwananchi huyo anapaswa kwenda polisi na nakala ya hukumu yake ili polisi waweze kushuhudia kwamba pande zote mbili ziliwahi kugombana kuhusu ardhi na kufikishana mahakamani lakini mmojawapo alishinda.
“Rais Magufuli alianzisha Mahakama ya mafisadi hapa nchini, kwa taarifa niliokua nayo, mahakama hii ina uhaba wa mafisadi, sasa mimi nitaitafutia wateja kwa kuhakikisha wale mafisadi ambao uonea wananchi, utesa wananchi, uiba fedha za serikali au taasisi yoyote nitawafikisha katika mahakama hiyo, hatutakubaliana na manyanyaso ya aina yoyote katika Serikali hii ya awamu ya tano” alisema Lugola.
Lugola aliongeza kua, hataki kusikia mwananchi anaonewa, na pia aliapa hatacheka na mafisadi, atapambana nao sehemu yoyote nchini na pia yupo tayari kwalolote na ameanza kupambana na mafisadi ndani ya wizara yake na tayari wameanza kurudisha fedha za Serikali.
Aidha, Lugola katika hotuba yake alipiga marufuku kwa waendesha bodaboda wenye tabia ya kubeba abiria zaidi ya mmoja kuiacha tabia hiyo ili kuepusha ajali, lakini aliwataka polisi kutorudi nyuma, wahakikishe wanawakamata waendesha bodaboda wasiofuata sheria za usalama barabarani.
Waziri Lugola yupo katika ziara jimboni kwake kwa kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuwaunganisha wananchi kupitia Bonanza lake la michezo ya mpira wa miguu ambalo linashirikisha kila kata wakitoa washindi mbalimbali ambao anawapa zawadi pamoja na kuingia moja kwa moja katika mashindano ya kugombea Kombe la Kangi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇