Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan amefariki dunia nchini Uswisi baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Bwana Annan alikuwa na umri wa miaka 80. Koffi Annan aliyekuwa katibu mkuu wa saba wa Umoja wa mataifa aliwahi kupewa tuzo ya kimataifa ya Amani ya Nobel mnamo mwaka 2001.
Taarifa kutoka kwa familia na kwenye wakfu wa Kofi Annan imetangaza kifo chake leo Jumamosi asubuhi.
Katika taarifa kupitia kwenye mtandao wa kijamii, taarifa hiyo ilisema"Kofi Annan, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na aliyewahi kupewa tuzo ya Amani ya Nobel ameaga dunia leo Jumamosi baada ya kuugua kwa muda mfupi."
Familia inaomba faragha wakati huu wa maombolezo na mipango ya kuenzi maisha yake pamoja na mipango ya msiba itatangazwa baadaye.
Mke wake bi Nane na watoto wao Ama, Kojo na Nina walikuwa pamoja naye wakati umauti ulipomfika.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema amesikitishwa sana na habari za kifo cha mtangulizi wake akimtaja kuwa alikuwa ni "nguvu iliyoongoza kwa mema".
Kofi Annan raia wa wa Ghana, aliyeishi nchini Uswisi, alikuwa mwanadiplomasia, mpole na mtulivu, alijulikana sana kwa kuongoza kwa uthabiti jumuiya hiyo ya ulimwengu katika siasa za kimataifa, tangu mwaka 1997 hadi 2006.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇