Na Felix Mwagara, MOHA
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kijiti cha kuiongoza Wizara yake alichokabidhiwa na aliyekua Waziri wa Wizara hiyo, Dkt Mwigulu Nchemba, atakikimbiza kwa kasi kwa kuwa yeye aliwahi kuwa mwanariadha.
Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya makabidhiano yaliyofanyika ofisini kwake, jijini Dodoma leo, Lugola alisema amekabidhiwa kijiti cha majukumu hayo mapya atahakikisha anasonga mbele kwa kutekeleza majukumu aliyopewa na Rais John Magufuli.
“Leo nimekabidhiwa ofisi, nimekabidhiwa zana alizokua anatumia Daktari wa Falsafa Mwigulu, pamoja na shughuli alizokua anazifanya mpaka hapa alipofikia, pia mimi niliwahi kuwa mwanariadha, na nilikua nashiriki mbio za kupokezana kijiti, na unapokabidhiwa kijiti, hautazami nyuma, ni kuendelea na safari,” alisema Lugola.
Pia Waziri Lugola alisema anapenda kuwaaambia Watanzania kuwa, atafanya kazi kwa kujiamini na yale mambo ambayo alielekezwa na Mheshimiwa Rais Magufuli kuyafanyia kazi, anaahidi atayashughulikia pamoja na majukumu mengine ya kiutendaji.
Kwa upande wake Dkt Mwigulu, alimpongeza Waziri Lugola kwa kuteuliwa kuwa Waziri, na pia alimtakia mafanikio katika uongozi wake na kumuhakikishia yupo tayari kutoa ushirikiano wowote ndani ya Wizara ili Tanzania iweze kusonga mbele.
“Leo nimemkabidhi Waziri Lugola Hotuba ya Bajeti ya Wizara ambayo ndiyo mwongozo wa Wizara kwa Mwaka wa Fedha huu tuliopo, na pia nimemkabidhi majukumu mengine ya kiutendaji niliyokua nayafanya,” alisema Dkt Mwigulu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akipokea taarifa ya makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Dkt Mwigulu Nchemba kwenye ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dodoma leo. Hata hivyo, Waziri Lugola alisema aliwahi kuwa mwanariadha, hivyo atahakikisha anasonga mbele kuendelea na safari, hata angalia nyuma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akipongeza na aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Dkt Mwigulu Nchemba mara baada ya kupokea taarifa ya makabidhiano kwenye ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dodoma leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimsikiliza Katibu wa Waziri Nelson Kaminyoge, alipokua anataka kumkabidhi taarifa aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Dkt Mwigulu Nchemba ilia aweze kukabidhiwa taarifa hizo. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisi ya Waziri huyo, jijini Dodoma leo.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akimuaga aliyekua Waziri wa Wizara hiyo, Dkt Mwigulu Nchemba, mara baada ya kukabidhiwa taarifa kwenye ofisi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dodoma leo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇