Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa imesema mamia ya raia wameuawa nchini Mali mwaka huu pekee, katika makabiliano baina ya makundi hasimu ya waasi.
Rupert Colville, msemaji wa ofisi hiyo amesema kwa akali raia 289 wameuawa katika matukio 99 ya mapigano baina ya makundi hasimu ya waasi au vita vya kikabila tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi sasa.
Amesema hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA); na kwamba asilimia 75 ya visa hivyo vimetokea katika eneo la Mopti, katikati mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa MINUSMA, aghalabu ya mapigano hayo ya kikabila huanzishwa na waasi wa kabila la Dozo (wawindaji wa asili), dhidi ya vijiji vya watu wa jamii ya Fulani.
Nchi ya Mali ilikumbwa na ghasia na ukosefu wa amani baada ya mapinduzi yaliyotokea nchini humo mwaka 2012.
Mwaka mmoja baadaye, Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MINUSMA) na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini humo kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu nchini humo huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇