LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 18, 2018

MAZUNGUMZO KATI VIONGOZI WA KIJESHI WA MAREKANI NA KOREA YA KASKAZINI

Wanajeshi wa ngazi ya juu wa Marekani na Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka 9 iliyopita wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu kurejesha mabaki ya miili ya wanajeshi wa Marekani waliouawa katika vita baina ya Korea mbili.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika kijijii cha Panmunjom katika eneo la mpaka kati ya Korea ya Kusini na ile ya Kaskazini. Mazungumzo hayo yamewakutanisha pamoja Jenerali Michael Minihan na ujumbe wa majenerali wawili kutoka Korea ya Kaskazini. Pande mbili hizo zimezungumzia suala la kuirejesha miili ya wanajeshi wa Marekani waliouawa katika vita kati ya Korea mbili. Kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa, Korea ya Kaskazini tangu mwaka 1990 imerejesha Marekani  mabaki ya miili 629 ya wanajeshi wa nchi hiyo waliouawa katika vita kuanzia mwaka 1950 hadi 1953. Rais Donald Trump wa marekani na Kim Jong -un Kiongozi wa Korea ya Kaskazini pia walikubaliana katika mazungumzo yao huko Singapore kuendelea kukabidhi mabaki hayo ya  miili  ya wanajeshi wa Marekani.  
Kiongozi wa Korea ya Kaskazini na Rais wa Marekani Donad Trump wakisaini makubaliano nchini Singapore
Kwa mtazamo wa serikali ya Pyongyang mazungumzo ya viongozi wa kijeshi wa Korea ya Kaskazini na Marekani katika uwanja huo yanafanyika katika kuendeza mchakato wa kuondoa hali ya mivutano kati ya nchi mbili hizo. Kwa kuzingatia hitilafu za kimitazamo zilizopo kati ya Korea ya Kaskazini na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kuhusiana na suala hilo; Pyongyang imetaka kufanyika mazungumzo katika ngazi ya wanajeshi kuhusu jambo hilo. Aidha kwa kutilia maanani kwamba kurejeshwa kwa mabaki hayo ya miili ya wanajeshi wa Marekani kutoka Korea ya Kaskazini ni suala la kibinadamu na lililo na taathira chanya kwa fikra za waliowengi nchini Marekani; Korea ya Kaskazini kwa kushirikiana katika uwanja huo inajaribu kuwaweka katika hali ngumu wale wote wanaopinga  huko Marekani kumalizwa hali ya mivutano na nchi hiyo ili kuendeleza upinzani wake. Matamshi ya Mike Pompeo Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani kwamba Korea ya Kaskazini  imeafiki kuanza oparesheni ya kuwatafuta karibu wanajeshi elfu tano wa Marekani waliopotea katika vita vya Korea mbili yanadhihirisha jitihada za Pyongyang za kujenga hali ya kuaminiana katika kushirikiana na Marekani. Kwa msingi huo, tovuti ya Korea ya Kaskazini kwa jina la Meari imetangaza kuwa nchi hiyo pia inataraji kuwa Marekani nayo itajenga hali ya kuaminiana; na iwapo nchi hiyo pia itachukua hatua katika mkondo sahihi; Korea ya Kaskazini nayo itachukua hatua nyinginezo mkabala wake ili kujenga hali ya kuaminiana kati ya pande mbili na kuzidisha uhusiano wa nchi hizo. Hii inamaanisha kuwa Korea ya Kaskazini inataka kutekeleza makubaliano ya Singapore bila ya tafsiri yoyote au matakwa ya kupenda makuu ya Washington. Hii ni kwa sababu katika siku za karibuni akiwa ziarani katika eneo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani alitoa matamshi na matakwa ambayo yameikasirisha Korea ya Kaskazini. Alidai kuwa Korea ya Kaskazini inapasa kusimamisha kikamilifu na kuihamishia nje ya nchi miradi yake ya nyuklia na kwamba miradi hiyo haipasi kuwa na uwezo wa kurudishwa katika hali yake ya awali. Hii ni katika hali ambayo Korea ya Kaskazini inaona kuwa mjadala uliopo sasa ni kuhusu kupokonywa silaha za nyuklia katika Peninsula ya Korea na si Korea ya Kaskazini.  
Mike Pompeo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani 
John Mirshermar Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Chicago anaamini kuwa Korea ya Kaskazini kivyovyote vile haitafumbia macho silaha zake za nyuklia kwa sababu kwanza kabisa nchi hiyo haiiamini hata kidogo Marekani na pili, Korea ya Kaskazini inaamini kuwa Marekani hadi sasa haijaheshimu hata kipengee kimoja cha makubaliano ya upokonyaji silaha za nyuklia iliyofikia na nchi hiyo.    
Kwa hali yoyote ile, Korea ya Kaskazini inaamini kutekeleza mpango huo na Marekani hatua kwa hatua kuhusiana na matukio yanayojiri katika Peninsula ya Korea. Imeitaka Washington ichukue hatua mkaba na hatua ili kufanikisha mpango wa kurejesha amani na uthabiti katika peninsula hiyo na makubaliano yaliyofikiwa huko Singapore ili kujenga hali ya kuaminiana kati ya pande mbili hizo na hivyo kusogeza mbele mambo kwa njia ya amani na bila ya uingiliaji wa mirengo yenye misimamo mikali ya Marekani. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages