LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 18, 2018

NDEGE YA WASAFIRI YA ETHIOPIA YATUA ERITREA BAADA YA MIAKA 20

Ndege ya kwanza ya kawaida ya wasafiri kutoka Ethiopia imetua katika mji mkuu wa Eritrea, Asmara, leo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20.
Ndege hiyo imelakiwa kwa shangwe kubwa ikiwa ni ishara ya kuzidi kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili za Pembe ya Afrika ambazo zilihasimiana kwa miongo miwili kabla ya kurejesha uhusiano wiki za hivi karibuni.
Mkurugenzi wa Shirika la Ndege la Ethiopia, Tewolde GebreMariam ambaye alikuwa ndani ya ndege hiyo aliwahutubia wasafiri punde baada ya kuingia katika anga ya Eritrea na kusema: "Hili linajiri kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20," huku akishangiliwa na abiria 315 waliokuwa ndani ya ndege hiyo.
Hayo yamejiri siku mbili tu baada ya Eritrea kufungua tena ubalozi wake nchini Ethiopia baada ya nchi hizo mbili jirani kumaliza uhasama wa miongoni miwili kuhusu mpaka.
Ubalozi wa Eritrea ulianza shughuli zake upya Jumatatu katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa katika sherehe iliyohudhuriwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na Rais wa Eritrea, Isaias Afwerki.
Rais Isaias Afwerki wa Eritrea (kushoto) na Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia
Kiongozi wa Eritrea aliwasili Addis Ababa Jumamosi iliyopita kwa safari ya siku tatu na alitembelea Ethiopia siku chache tu baada ya Abiy Ahmed kutembelea mji mkuu wa Eritrea, Asmara ambapo wawili hao waliafiki kuanzisha tena uhusiano wa kidiplomasia.
Eritrea ilijitenga na Ethiopia mwaka 1993  na kukata uhusiano wa pande mbili na hivyo kupelekea Ethiopia ikose njia ya bahari. Mwaka 1998 kuliibuka vita vikali na mzozo wa mpakani baina ya nchi hizo ambao ulipelekea watu zaidi ya 80,000 kupoteza maisha na malaki kuachwa bila makazi.
Mwaka 2000 Umoja wa Mataifa ulizipatanisha pande mbili hizo na kusema eneo la mpakani lililokuwa likizozaniwa ni milki ya Eritrea lakini mapatano hayo ya amani hayakutekelezwa baada ya Ethiopia kuyapinga. Hatimaye mwezi uliopita wa Juni Waziri Mkuu wa Ethiopia aliwashangaza wengi alipokubali mapatano hayo ya amani na hivyo kuhitimisha uhasama baina ya pande mbili hizo.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages