Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetangaza kuwa, kuna uwezekano mkubwa wa kutokomezwa maradhi ya Ebola nchini humo ifikapo Julai 25, 2018.
Taarifa ya wizara hiyo imebainisha kwamba, nchi hiyo inasubiri kwa hamu tarehe 25 ili kutangaza kutokomezwa kwa ugonjwa wa Ebola nchini humo iwapo kutakuwa hakujaripotiwa kesi mpya ya maambuzi ya ugonjwa huo.
Hii inatokana na ukweli kwamba, tangu tarehe 12 mwezi uliopita hadi jana hakuna kisa chochote kipya cha Ebola kilichoripotiwa na hivyo ikifika tarehe 24 mwezi huu bila kuripotiwa kesi mpya ya ugonjwa huo basi vita dhidi ya mlipuko wa Ebola ulioanza tarehe 8 mwezi Mei mwaka huu vitakuwa vimefanikiwa, imeeleza sehemu nyingine ya taarifa hiyo.
Akizungumza na waandishi habari mjini Geneva, Usiwisi, Fadela Chaib msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) amesema kuwa, wizara husika itatoa maelezo zaidi baadaye.
Amesema, Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia mapendekezo kutoka WHO, inapanga Julai 24 kuwa ndio mwisho wa mlipuko wa Ebola na itatoa tangazo rasmi Julai 25.
Mlipuko mpya wa ugonjwa wa Ebola ulianza tarehe 8 Mei mwaka huu katika mji wa Bikoro kwenye mkoa wa Équateur huko kaskazini magharibi mwa Congo na baadaye maambukizi ya ugonjwa huo yalihamia katika mji wa Mbandaka ambao ndio makao makuu ya mkoa huo.
Itakumbwa kuwa, kuanzia mwishoni mwa mwaka 2013 hadi 2016 ugonjwa huo ulisababisha vifo vya zaidi ya watu elfu 11 na 300 katika baadhi ya nchi za magharibi mwa Afrika.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇