LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 25, 2018

MPIGAPICHA MSTAAFU WA MAGAZETI YA UHURU NA MZALENDO AFARIKI DUNIA

Dar es Salaam
Mpigapicha mashuhuri mstaafu wa kampuni ya magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru Publications Ltd, wachapishaji wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani Mzee Mwalimu Omary (pichani) amefariki dunia leo alfajiri Julai 25, 2018, akiwa na umri wa miaka 86.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 25, 2018 na mtoto mkubwa wa marehemu, B Omary Mwalimu Omary imesema Mwalimu Omary amefariki leo alfajiri Julai 25, 2018 wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali na Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kampasi ya Mloganzila, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam

“Mzee alianza kulalamika kuumwa tumbo wiki mbili zilizopita na kufuatiwa na kupooza mkono na mguu, ambapo kabla ya kufikishwa hapa Mloganzila, Mzee tulimpeleka hospitali za Magomeni Mapipa na kuhamishiwa Mwananyamala kabla ya kuletwa huku Mloganzila  kufanyiwa vipimo vya kichwa.” Alisema.

Bw. Omary alisema, Mwalimu Omary ambaye alifanya kazi kwa miaka mingi kwenye magazeti ya Uhuru na Mzalendo, alipata nafuu kidogo na aliweza hata kuzungumza nae.

“Nakumbuka mara ya mwisho (jana Julai 24, 2018) Mzee aliniambia nimletee fulana yake iliyoandikwa Uhuru na Mzalendo, na kweli nilikuwa nimemchukulia leo hii, lakini nilipofika nikakuta kitanda chake kiko tupu, na baada ya kuuliza nikaambiwa na manesi pole, mzee ametutoka,” Alisema Bw. Omary katika mahojiano kwa njia ya simu.

Aidha Bw. Omary amesema, mipango ya mazishi inafanywa nyumbani kwa marehemu Mburahati jijini Dar es Salaam.

Mwalimu Omary ameacha mke, watoto wanne na wajukuu 11.

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages