Na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Suzan Mlawi amesema kuwa Dodoma ni nzuri kwani haina msongo wa mawazo (stress) kwa watumishi kutokana na miundombinu ya barabara zisizo na msongamano.
Bibi Mlawi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na watumishi wa wizara hiyo waliohamishiwa Dodoma.
“Nipende kuwahakikishia watumishi wenzangu kuwa Dodoma hukuna stress ni sehemu ambayo kuna utulivu wa akili (Peace of mind) kwani hakuna kuamka usiku sana kukimbizana na magari na kuwaza foleni wakati wa kurudi nyumbani”, alisema Mlawi.
Wakati Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli akitangaza kuwa Serikali inahamia Dodoma watu wengi wakiwemo watumishi wa Serikali hawakufurahishwa na uamzi huo, lakini baada ya kuhamia, wengi wao wamepapenda na kusema kumbe Dar waliizoea tu na kuamini kuwa kuamka usiku sana kukwepa foleni ili wawahi kazini kwamba lilikuwa jambo la kawaida.
Baada ya kuhamia Dodoma na kuona kuwa hakuna ulazima wa kuamka usiku ili uwahi kazini wametokea kulipenda sana jiji hilo na kuukubali uamzi wa Mhe. Rais Magufuli.
Kwa sasa kinachoendela nje ya kazi ni watumishi hao kupigana vikumbo wakitafuta viwanja ili wafanye makazi na shughuli za ujasiriamali wenye tija.
Kwa wale ambao wana muda mrefu jijini Dodoma baada ya kuhamia rasmi wamesikika wakisema kuwa Dodoma ni sehemu nzuri ya kukaa kwani hali ya maisha ni ya wastani na mtu anaweza kupanga ratiba yake na kuitekeleza kwani hakuna ambako atakutana na msongamano wa magari.
Hapa amesikika Mkurugenzi Msaidizi wa Shughuli za Maktaba ya Bunge, Deogratias Egidio akisema kuwa tangu amehamia Dodoma hana stress zinazotokana na kuchoshwa na kukaa barabarani muda mrefu kutokana na msongamano wa magari.
Ameongeza kuwa na hali ya hewa ni nzuri kwani kuna ubaridi na joto la wastani ambavyo havimfanyi mtu kukereka.
Kiafya, uwezekano wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya kwa Dodoma inawezekana kabisa mtu kuamka mapema na kufanya mazoezi hata baada ya kutoka kazini.
Mapema mwezi jana, Mbunge wa Kibakwe (CCM), Mhe. George Simbachawene amewasilisha azimio la kuitaka Serikali kuharakisha mchakato wa Muswada wa Sheria ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu na kuuleta bungeni.
Akiwasilisha azimio la kumpongeza Rais John Magufuli kwa uamuzi wake wa kuendeleza mji wa Dodoma na kuupa hadhi ya jiji, bungeni, Simbachawene alisema ikiwezekana Muswada huo usomwe mara ya kwanza katika mkutano wa 11 uliokuwa ukiendelea."Naiomba Serikali kuongeza raslimali fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali itakayoendana na hadhi ya makao makuu na jiji kama vile ujenzi wa Barabara zenye kiwango, miundombinu ya Reli, Gesi na Umeme.
Uamzi wa kuhamishia makao makuu Dodoma ulitolewa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1973. Utekelezaji uliendelea kwa kasi ndogo hadi mapema mwaka 2016 wakati wa sherehe ya kumbukumbu ya mashujaa iliyofanyika Dodoma ambapo Rais Magufuli alitamka rasmi kuwa Serikali inahamia Dodoma. Miezi miwili baadae, Mhe. Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alihamia Dodoma na mwaka jana Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan naye akahamia.
Kwa sasa zoezi la Serikali Kuu kuhamia Dodoma karibu limekamilika kwani watendaji wakuu wa Serikali wakiwemo mawaziri, manaibu na makatibu wakuu na wakurugenzi wameshahamia Dodoma na watumishi wengi wa serikali.
Mwaka huu kabla haujaisha, Mhe. Rais John Pombe Magufuli naye anatarajiwa kuhamia Makao Makuu Dodoma ambalo sasa limekuwa jiji.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇