Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Dk. Edmund Mndolwa akizungumza na Viongozi wa Jumuiya hiyo, leo mjini Tarime mkoani Mara. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Erasto Sima, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo mkoa wa Mara Samweli Kiboya na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania uoande wa Zanzibar Haidar haji Abdallah na kulia ni Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara Mrida Mshota.
Na Bashir Nkoromo, Tarime
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania Dk. Edmund Mndolwa ameshangazwa na baadhi ya wanachama wa CCM na Jumuiya zake kushindwa kulipa ada ya uanachama ya sh. 1200 kwa mwaka, ambayo ni sawa ya bei ya soda moja.
Dk. Mndolwa ameelezea kushangazwa huko, wakati akizungumza na viongozi wa CCM na Jumuiya za CCM kutoka Wilaya za mkoa wa Mara, katika ukumbi wa CMG mjini Tarime, leo, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.
Kufuatia hali hiyo Dk. Mndolwa ameagiza viongozi kusimamia ipasavyo ili kuhakikisha kila mwanachama wa CCM na Jumuiya ya Wazazi Tanzania analipa ada yake ya kila mwezi, akisisitiza kuwa watakaoshindwa kufanya hivyo itakuwa ni mfano unaoonyesha kuwa hawafai uongozi kutokana na kushindwa kusimamia uhai wa Jumuiya hiyo na Chama Cha Mapinduzi.
"Unamkuta mtu kila mara anajinasibu kuwa ni mwanachama wa CCM au Jumuiya ya Wazazi, lakini wakati huo huo halipi ada ya uanachama ya kila mwaka mbayo gharama yake kwa kila mwaka ni sawa na bei ya soda moja ambayo kila siku anamudu kuinunua", alisema Dk. Mndolwa.
Alisema, ni jambo la muhimu kwa kila mwanachama kuhakikisha analipa ada yake ya uanachama kwa sababu kufanya hivyo ndiyo ishara pekee inayodhihirisha uanachama wake kwa kuwa asipofanya hivyo anakuwa mwanachama mfu asiyeshiriki katika kuimarisha uhai wa Chama.
Dk. Mndolwa amewasisitiza wanachama wa CCM kujiunga na Jumuiya za Chama akisema kwamba kufanya hivyo kunatoa fursa pana zaidi kwa mwanachama kuijenga CCM na pia hata kuwea kupata nafasi za uongozi kwa wepesi zaidi kuliko akiwa mwana CCM tu.
"Tazameni, hivi sasa mimi ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM lakini ni kwa sababu nimekuwa mwanachama wa Jumuiya ya Wazazi na kisha nikagombea kupitia huko na kupata Uenyekiti wa Jumuiya hii ambapo sasa kwa nafasi niliyo nayo ya Uenyekiti nimekuwa pia Mjumbe wa Kamati Kuu", alisema Dk. Mndolwa.
Akizungumzia maadili katika jamii, Dk. Mndolwa aliwatupia lawama wazazi kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha kumomonyoka kwa maadili katika jamii kutokana na kuwaacha watoto wao kufanya wapendavyo katika masuala ya tabia.
"Unakuta binti anatoka nyumbani amefaa nguo za kubaka maungo na zinazoacha wazi baadhi ya maungo yanayostahili kusitiriwa, mzazi anaona lakini anamuacha bila kumkemea, matokeo yake binti anakuwa mitaani katika namna ya kutokuwa na maadili bora, ikitokea hivyo jua lawama ni kwa mzazi", alisema Dk. Mndolwa.
Alisema, hali kadhalika ni kosa la mzazi pale mtoto wa kiume anapotoka nyumbani huku amevaa katula au suruali inayoporomoka matakoni, kwa sababu mzazi anapaswa kukemea uvaaji huo kwa kuwa unatia aibu katika jamii.
"Unakuta mzazi anampa hela nyingi mtoto wakati anakwenda shuleni huku akisema kuwa kwa kuwa yeye alisoma katika mazingira ya taabu hataki mwanae asome kwa taabu, kumbe hajui kuwa kwa kufanya hivyo anamjengea mtoto vishawishi vya kutumbukia katika utumiaji wa dawa za kulevya na uvutaji bangi", alisema Dk. Mndolwa.
Dk. Mndolwa aliwataka wazazi kuwa mstari wa mbele kuwahakikisha wanasaidia kujenga maadili ya jamii kwa kuwakanya na kuwachukulia hatua thabiti watoto wao kila wanapowagundua au kuwaona wanajaribu kuanza kuiga tabia zinazomomonyoa maadili.
Akizungumzia mshikamano ndani ya Chama, Dk. Mndolwa aliwataka wana CCM kuachana kabisa na mtindo wa kung'ang'ania makundi kila baada ya uchaguzi na pia kuachana na tabia ya kuthani mtu fulani ni maarufu kuliko chama.
Dk. Mndolwa alisema, ikiwa wanachama wataachana na mambo hayo CCM inakuwa imejihakikishia kupata ushindi kila uchaguzi kwa kuwa inao wanachama na wapenzi wengi na kinachohitajika ni mshikamano tu.
"Hadi sasa kuna baadhi ya majimbo au Kata walizoshinda wapinzani katika uchaguzi uliopita, lakini kwa maoni yangu wapinzani hawakushinda maeneo hayo eti kwa sababu ni weledi sana, hapana. ukweli ni kwamba walishinda kwa sababu ya uzembe wa wana CCM wenyewe kung'ang'ania makundi baada ya kura za maoni", alisema Dk. Mndolwa.
Lengo la ziara hiyo ya Dk. Mndolwa katika mikoa ya Kanda ya ziwa na mkoa wa Singida, ni kuwashukuru wananchama wa Jumuiya ya Wazazi kwa kumchagua kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na pia kuwatambulisha Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Tanzania kwa upande wa Zanzibar Haidar Haji Abdallah na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Erasto Sima ambao ameambatana nao katika ziara hiyo.
PICHA ZA ZIARA YA DK. MNDOLWA MKOANI MARA>BOFYA HAPA
Your Ad Spot
Jun 11, 2018
Home
Unlabelled
DK. MNDOLWA: MNASHINDWAJE KULIPA ADA YA UANACHAMA YA KILA MWAKA AMBAYO GHARAMA YAKE NI SAWA NA SODA MOJA?
DK. MNDOLWA: MNASHINDWAJE KULIPA ADA YA UANACHAMA YA KILA MWAKA AMBAYO GHARAMA YAKE NI SAWA NA SODA MOJA?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇