NA BUSHIR MATENDA- MAELEZO
Serikali
ya Tanzania imepongezwa kwa jitihada zake za kukabiliana na mashambulizi dhidi
ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) ambazo zimepelekea kupungua kwa kiasi
kikubwa cha vitendo hivyo vya kikatili dhidi yao.
Akiwasilisha
Taarifa ya Utafiti wake, Mtaalamu wa Kujitegemea kuhusu kunufaika na haki za
binadamu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi, Mtaalamu wa kujitegemea Bi. Ikponwosa
Ero amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kushughulikia kadhia
inayowapata watu wenye ulemavu wa ngozi.
“nimefurahishwa
na taarifa ya kupungua kwa idadi ya mashambulizi yaliyoripotiwa na naipongeza
Serikali ya Tanzania kutokana na juhudi zake
kushughulikia tatizo hilo” alieleza Mataalamu huyo.
Aliongeza
kuwa hatua za Serikali za kukabiliana na vitendo vya ushirikina ambavyo ndio
kichocheo kikubwa cha vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi
hazina budi kuambatana na kutolewa elimu zaidi kwa jamii ili waache imani
potofu dhidi ya matumizi ya viungo vya watu wenye ulemavu wa ngozi katika
kupata utajiri.
Hata
hivyo aliwaeleza waandishi wa habari kuwa pamoja na kupungua kwa vitendo vya
mashambulizi dhidi ya watu hao lakini bado watu wenye ulemavu wa ngozi
wanaendelea kuishi kwa hofu kwa kuwa chimbuko la ukatili huo bado lipo.
“Watu
wenye ulemavu wa ngozi pamoja na maswahiba mengine ya kimaisha kama umasikini
na ukosefu wa elimu lakini bado wanaendelea kuishi kwa hofu hususan katika
maeneo ya vijijini” alisema Bi Ero.
Bi.
Ero, raia wa Nigeria, ambaye ni mmoja wa watalaamu wa haki za biandamu wa Umoja
wa Mataifa, alieleza kutiwa moyo hali ya ushirikiano uliopo kati ya Serikali na
wadau wengine wakiwemo Umoja wa Mataifa na Asasi za Kiraia hali ambayo
imesaidia sana Tanzania kupata mafaniko kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya
albino.
“Ni
faraja kubwa kuona Serikali inafanya kazi bega kwa bega na asasi za kiraia
katika sekta ya elimu na afya, hasa katika kuwapatia vifaa vya kuonea pamoja na
kuanzisha huduma za kliniki kwa magari ili kuzuia kansa ya ngozi” alibainisha
Bi. Ero
Mtaalamu
huyo ambaye aliwasili nchini tarehe 18 Julai, 2917 alibainisha kuwa akiwa
nchini alipata fursa ya kutembelea mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma,
Shinyanga na Mwanza ambako alionana na watu mbalimbali kutoka Serikalini, asasi
za kiraia, watu walioathirika na vitendo dhidi ya maalbino pamoja na familia
zao.
Katika
utafiti huo ambao anatarajia kuuwasilisha katika Baraza la Haki za Binadamu la
Umoja wa Mataifa mwezi Machi mwakani, Bi Ero alieleza kuwa bado jitihada zaidi
zinahitajika katika kuelimisha wananchi kuhusu hali ya watu wenye ulemavu wa
ngozi ili waweze kuwakubali warudipo katika jamii baada ya kuishi kwenye kambi
maalum ikiwemo watoto wanaoishi katika shule za bweni.
“Nina
wasiwasi kuwa makambi hayo yaliyoanzishwa kwa muda yanaonekana kuwa sasa
yamageuzwa kuwa makaazi ya kudumu kwa watu hao kwa kuwa bado jamii
haijawakubali kwa hivyo wanasita kuwapokea”
Nae
Mratibu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilishi
Mkaazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Alvaro
Rodriguez ameishukuru Serikali ya Tanzania chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Mh. John pombe Magufuli kwa kumruhusu Mtaalamu huyo wa kujitegemea
kuja kufanya tafiti utafiti huo.
Alibaisha
kuwa hatua hiyo ya Serikali inadhihirisha dhamira yake ya kushughulikia kwa
dhati changamoto mbali mbali zinazowakabili watu wenye ulamavu wa ngozi nchini.
Bwana Rodriguez
amepongeza jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali katika kuhakikisha watu
wenye ulemavu wa ngozi wanakuwa salama muda wote katika jamii zao na jitihada
endelevu ya kuboresha mambo muhimu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ikiwemo
vifaa vya kuona, huduma bora ya Afya na kuwaendeleza katika elimu.
Bi. Ero aliwasili nchini 2017 akifanya tathmini
juu ya hali ya haki za binadamu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kwa
kujizangatia jitihada zinazofanywa na Serikali na wadau mbalimbali kuboresha
ustawi na haki zao.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇