NA MWANDISHI MAALUM
Aakiitikia agizo la Rais John Pombe Magufuli
alilowataka wateule wake kuwa wabunifu na kujituma ili kuwaondolea wananchi
shida mbalimbali , Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ametatua
migogoro takribani 8, 000 iliyowahusisha zaidi ya watu 80, 000 ndani ya
takribani miezi minane kati ya Disemba mwaka jana na Mwezi Juni mwaka huu.
Makonda ametekeleza jukumu hilo kupitia timu
ya wanasheria 35 wanaojitolea kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa
wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam.
Kiongozi wa timu ya Wanasheria hao, Georgia
Kamina, aliitaja baadhi ya migogoro ambayo timu yake imekuwa ikisuluhisha
kupitia Ofisi za Wakuu wa Wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam kuwa ni ile ya
umiliki wa ardhi na michakato ya mirathi mahakamani na katika ngazi ya familia,
Migogoro mingine ambayo timu hiyo ya
wanasheria imekuwa ikimsaidia Makonda kuitatua kwa kushirikiana na Wakuu wa
wilaya ya Ilala (Sofia Mjema), Kinondoni (Ally Hapi), Temeke
( Felix Lyaniva ), Ubungo (Kisare Makori ) na Kigamboni
(_Hashimu Mgandilwa ) ni pamoja na ndoa na matunzo ya watoto kwa ndoa
zilizo sambaratika, ajira na mikataba ya ajira, ubakaji, faili kupotea
mahakamani, ucheleweshwaji wa kesi mahakamani, umiliki wa nyumba, umiliki
au mauziano ya ardhi, mikopo kutoka mabenki ya biashara, uuzwaji mali
mbalimbali kwa kukiuka sheria au makubaliano na hata ukosefu wa uaminifu.
Akizungumza kwa niaba ya Makonda, katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Ilala Boma, Kamina, alitaja migogoro wanayopokea na inayotia fora katika mkoa wa
Dar es Salaam kuwa ni ile inayohusisha masuala ya mirathi, umiliki wa
ardhi, ajira na mikataba kati ya waajiri na waajiriwa, ndoa na matunzo ya
watoto kwa ndoa zilizo sambaratika na baadhi ya wananchi kuingia mikataba
mibovu na mabenki katika harakati za kupata mitaji ya biashara.
Sehemu ya Jiji la Dar es Salaam |
"Mheshimiwa Paul Makonda alichukua
jukumu la kuanzisha huduma ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi
kutokana na uzoefu alioupata katika ziara ya kukutana na wananchi aliyofanya
mkoa mzima mwezi Novemba mwaka jana," alibainisha Kamina na kuongeza kuwa
ili kuwaepusha wananchi na mchakato mrefu na unaoumiza wa kumaliza migogoro yao
mahakamani aliamua kuunda timu ya wanasheria wa kujitolea ili kutekeleza
dhamira hiyo ya kuwasaidia wananchi wenye migogoro mbalimbali ya kisheria.
Kiongozi wa timu ya wanasheria hao aliongeza
kwa kusema kuwa Mkuu wa Mkoa aliguswa na namna baadhi ya wananchi walivyokuwa
wakipoteza mashamba, nyumba, mali na hata kufukuzwa kazi kwa uonevu kwa kukosa
uelewa wa sheria.
“Ili kupata suluhisho la matatizo hayo hapo
juu na kwakuwa yeye binafsi akiwa msaidizi wa Rais kwa mkoa wa Dar es Salaam
basi ndio akaja na wazo la kuanzisha kitengo cha kutatua migogoro ya kisheria
kwa njia ya kutoa huduma ya msaada kisheria bila malipo kwa wananchi katika
kila wilaya ya mkoa wa Dar es Salaam.
"Tupo jumla ya wanasheria 35 ambao
tumegawanyika katika Wilaya zote za mkoa wa Dar es Salaam yaani Ilala,
Kinondoni, Temeke, Ubungo na Kigamboni. Tukiwa katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya
nilizotaja tunafanya kazi nao kwa karibu sana na pengine wakati mwingine
tunajumuika na Makatibu Tawala wa Wilaya husika (DAS) na hata
wakati mwingine Wakurugenzi Watendaji wa manispaa za mkoa wa Dar es Salaam
katika kutatua migogoro hiyo kisheria,” alifichua Mkuu huyo wa Timu ya
Wanasheria.
Akizungumzia uzoefu waliopata katika kipindi
cha miezi saba walichofanya kazi ya kutoa huduma ya msaada wa kisheria bure
kwa wananchi kwa kusuluhisha migogoro mbalimbali wamegundua wananchi
wengi ama hawana au wana uelewa mdogo wa sheria na kila wakati wanafanya makosa
makubwa ya kisheria yanayoishia kuwaumiza kimaisha.
"Kuna kina baba na kina mama wengi tu
wamekuja mara baada ya kunyang'anywa nyumba zao na mabenki kutokana na kukubali
kutoa hati za nyumba hizo kudhamini mikopo ya jamaa zao wakiamini kuwa kama
kutakuwa na kutokuelewana kati ya mabenki na ndugu zao nyumba hizo hazitauzwa
jambo ambalo sio kweli," alisimulia Kamina.
Akitaja baadhi ya migogoro iliyowagharimu muda
na juhudi za ziada kuisuluhisha, Kamina alitaja mgogoro wa umiliki wa ardhi ya
hekari 28 unaomhusisha Ogwari Nashon na wakazi wa kijiji cha Viwege, Mbondela
eneo la Chanika katika Wilaya ya Ilala.
“Mgogoro huu ulifika mahala ukahatarisha
maisha ya ndugu Nashon kwani baadhi ya wanakijiji wasioheshimu sheria walivamia
eneo lake, kuchoma moto majengo na kuharibu mazao kama mihogo, mananasi na
michungwa.
Mara baada ya Nashon kuja ofisi ya Mkuu wa
wilaya ya Ilala alikutanishwa na wanasheria wa Mkuu wa Mkoa
wanaotoa huduma ya msaada wa kisheria bure kwa wananchi walioko
wilayani hapo na kueleza tatizo lake ambapo timu yetu iliingilia kati kwa
kushirikiana na Mkuu wa wilaya ya Ilala Sofia Mjema, ili kupata ufumbuzi wa
mgogoro huo.
Ni jambo la kutia faraja kwa sasa tumepiga
hatua kubwa kuelekea kutatua mivutano iliyokuwepo kwani Nashon ana vielelezo
halali vya nyaraka za kiserikali zinazothibitisha umiliki wa eneo hilo,"
alibainisha Kamina.
Licha ya kujitokeza picha nzuri iliyojaa mafanikio ya huduma hii
ya msaada wa kisheria kwa wananchi katika Mkoa wa Dar es
Salaam, Habari Leo imearifiwa juu ya changamoto lukuki zinazowakabili watoa
huduma hiyo katika kutekeleza majukumu yao.
Baadhi ya changamoto hizo ni wananchi kutokuwa na uelewa wa
sheria, kanuni na taratibu za kukopa fedha kwa watu binafsi na katika taasisi
za fedha, wananchi hawana uelewa wa sheria na taratibu za mirathi na hata
wasimamizi wa mirathi hawajui wajibu wao kwa warithi na kwa mahakama jambo
ambalo linapelekea warithi kuchelewa au kutopatiwa haki zao hata baada ya
mchakato wa mirathi kukamilika katika Mahakama.
“Katika eneo la ajira huko ndio kunatisha kwa uvunjaji wa sheria
za ajira na nchi uliokithiri kwani makampuni mengi hasa ya ujenzi na ulinzi
hayatoi mikataba ya ajira kwa wafanyakazi, wakati mwingine mikataba inakuja
kutolewa baada ya mwajiriwa kuwa amekwisha fanya kazi muda mrefu na inapotolewa
inakuwa inakiuka makubaliano ya awali,” alisema na kuwanyooshea kidole viongozi
wa serikali za mitaa na kata, katika baadhi ya maeneo kwa kuwa chanzo cha
migogoro kwa kufanya majukumu ambayo si yao kisheria na uendeshwaji wa kesi
mahakamani kuchukua muda mrefu pasipo na sababu za msingi huku Mabaraza ya kata
nayo kuwa dhaifu katika kutekeleza majukumu yake ya kimsingi katika kuwahudumia
wananchi na hasa wale wa kipato cha chini.
Akizungumzia huduma hiyo, Makonda alisema aliamua kuanzisha
huduma ya msaada wa kisheria kupitia wanasheria hawa (35) katika kila wilaya ya
mkoa wa Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama tawala
Chama Cha Mapinduzi (CCM) inayoagiza kusikiliza na kutatua kero au malalamiko
ya wananchi.
Mkuu huyo wa Mkoa alifafanua kuwa katika ziara ya mkoa wa Dar es
Salaam mwishoni mwa mwaka 2016 aligundua wananchi wengi hawakuwa na
uelewa wa sheria jambo lililowafanya kupoteza haki zao aidha kwa kutapeliwa,
kuonewa au kutojua mahala sahihi pa kupeleka matatizo hayo.
"Pamoja na changamoto nyingi zinazoambatana na huduma hii
ya kutafuta suluhu ya matatizo ya wananchi kwa kuzileta pande husika mezani
kuongea bado nina dhamira ya kuendelea kuwasaidia Watanzania wenzangu kwa
juhudi na maarifa yangu yote.
Na hii ndio gharama ya kuteuliwa na Rais,
unapoteuliwa na Mkuu wa nchi anakuwa na matarajio mengi kutoka kwako. Mimi
nimeamua kufanya ninayoweza kwa nguvu na juhudi zote ili kumuondolea Rais John
Pombe Magufuli na mashinikizo juu ya shida mbalimbali za Wana Dar es
Salaam," alimaliza Makonda.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇