Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza
taasisi za Serikali na taasisi binafsi zinazotumia mifumo ya kielektroniki
kujiunga na mfumo wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki (Electronic Revenue Collection System {e-RCS})
ili kupata taarifa za uhakika na kulinda usalama wake pamoja na kuiwezesha
Serikali kukusanya mapato yote stahiki.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 01 Juni, 2017 alipotembelea Kituo
cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu (National
Internet Data Center) kilichopo
Kijitonyama Jijini Dar es Salaam na kisha kuzindua mfumo wa ukusanyaji wa kodi
kwa njia ya kielektroniki uliotengenezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa kutumia wataalamu wa ndani.
Uzinduzi
huo umehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.
Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu Hassan, Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Tanzania Bara na Zanzibar na
wadau mbalimbali wakiwemo wawakilishi kutoka benki mbalimbali, kampuni za simu
na viongozi wa dini.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Kamishna
Mkuu wa TRA Bw. Charles Kichere kuwa mpaka sasa ni kampuni tatu za simu ambazo
ni TTCL, Halotel na Smart ndizo zimejiunga kutumia Mfumo huu na kwamba TRA na
ZRB zinatarajia kampuni zote za simu, mabenki na taasisi mbalimbali kujiunga na
mfumo wa e-RCS kabla ya mwisho wa mwaka 2017.
“Wanaokusanya
mapato wanalalamika kuwa kumekuwa na udanganyifu kwenye utoaji taarifa za
wafanyabiashara na wafanyabiashara nao wanalalamika kuwa wamekuwa
wakibambikizwa kodi, sasa dawa ya haya yote ni Kituo hiki cha Taifa cha
Kuhifadhi Kumbukumbu, jiungeni na mfumo huu kwa sababu sasa kila kitu
kinafanywa na mashine, hakuna kuonea mtu, na Mhe. Makamu wa Rais naomba
usimamie suala hili” amesema Mhe. Rais
Magufuli.
Pamoja
na kutoa agizo hilo Mhe. Dkt. Magufuli ametaka taasisi zote za Serikali zenye
vituo vya kumbukumbu (Data Centers)
kuoanisha vituo hivyo na amepiga marufuku kuendelea kuanzisha vituo vingine, na
badala yake zitumie Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuzibana kampuni zote za simu
ambazo hazijajiunga na soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) kujiunga haraka ili kuwepo uwazi katika uendeshaji wake huku
akisisitiza kuwa Serikali inawapenda wawekezaji lakini ni lazima walipe kodi
inavyostahili kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi.
Kwa
upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali
Mohamed Shein ameungana na Rais Magufuli kuzipongeza TRA na ZRB kwa kuanzisha mfumo
wa ukusanyaji wa kodi kwa njia ya kielektroniki na amewataka Watanzania wote kulipa
kodi ili kuinua uchumi.
“Natoa
pongezi kwa kuanzishwa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Kumbukumbu, kituo hiki ni ‘State of the Art’ nakupongeza pia Mhe. Rais Magufuli kwa kuwa
tangu uingie madarakani umetia msisitizo mkubwa katika kuongeza ukusanyaji wa
kodi, na kwa kweli ukusanyaji wa kodi umeongeza” amesema
Mhe. Rais Shein.
Gerson
Msigwa
Mkurugenzi
wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar
es Salaam
01
Juni, 2017
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇