LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jun 29, 2017

RAIS DK MAGUFULI ATUMA SALAM ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA MKURUGENZI MKUU AfDB

DAR ES SALAAM, TANZANIA
Rais Dk. John Magufuli ametuma salam za rambirambi kufuatia kifo cha Mkurugezi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) Dk. Tonia Kandiero.

“Kwa mshituko na masikitiko makubwa nimepokea taarifa za kifo cha Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) katika Kanda ya Afrika Kusini Dk. Tonia Kandiero aliyefariki dunia ghafla jana usiku tarehe 28 Juni, 2017 akiwa ofisini kwake huko Pretoria Afrika Kusini”

Hii ni kauli ya Dk. John Magufuli aliyoitoa leo, Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa za kifo cha Dk. Tonia Kandiero ambaye kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa AfDB katika Ofisi za Kanda ya Afrika Kusini mwishoni mwa mwaka 2016 alikuwa Mwakilishi wa AfDB Tanzania.

Taarifa ilyotolewa na Ikulu jijini Dar es Salaam, imemkariri Rais Dk. Magufuli akisema, “Nitamkumbuka Dk. Tonia Kandiero kama mchapakazi hodari aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu, nikiwa Waziri wa Ujenzi nimeshirikiana nae kwa karibu kufanikisha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo kwa nchi yetu ambayo imefadhiliwa na AfDB, ametoa mchango mkubwa kufanikisha ujenzi wa madaraja na barabara za Dodoma – Iringa, Dodoma – Babati, Namtumbo – Tunduru – Mtambaswala, Arusha – Taveta – Voi na pia alitoa mchango mkubwa katika kufanikisha miradi mingine ambayo ipo mbioni kutekelezwa ikiwemo ujenzi wa barabara ya Bagamoyo – Tanga – Mombasa, Mbinga – Mbambabay na Tabora - Katavi”.

Kufuatia kifo cha Dk. Tonia Kandiero Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Rais wa AfDB Dkt. Akinwumi Adesina, familia ya Dk. Tonia Kandiero, wafanyakazi wote wa AfDB, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu na  amemuombea marehemu Dk. Tonia Kandiero apumzishwe mahali pema peponi.

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages