Utambuzi
wa historia ya nchi una mchango mkubwa kwa vijana kuweza kufahamu madhila yaliyotokea
na jinsi viongozi walivyopigana katika kuleta uhuru na maendeleo ya Taifa.
Katika makala haya Judith Mhina wa Idara ya Habari MAELEZO anaelezea.
Waziri
Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Kwanza na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Dkt
Salim Ahmed Salim amesema kuwa vijana barani Afrika wana wajibu wa kujua
historia ya nchi na viongozi waliojitolea kuleta uhuru, umoja, amani na maendeleo
ya watu.
Amesema,
athari za vijana kutojua historia ya nchi na viongozi waliopigania uhuru ni
pamoja na kukosa uzalendo na uwajibikaji katika kutekeleza malengo ya Serikali
katika kuleta mapinduzi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii jambo ambalo
linarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Ameeleza
kuwa, nafasi waliyonayo kama vijana ni kujifunza jinsi viongozi wetu
walivyoweza kuweka misingi ya umoja, amani, mshikamano na changamoto zilizowakabili
na jinsi walivyoweza kuzitafutia ufumbuzi badala ya kukata tamaa na kuilaumu Serikali
kuwa haiwasaidii.
Dkt
Salim amefafanua kuwa nchi yetu imeonyesha muelekeo mzuri katika kulikomboa kundi kubwa la vijana kuelekea kwenye
uchumi wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. “Mimi binafsi naipongeza
Serikali yetu kwa kuonesha nia njema ya kupunguza au kuondoa changamoto,
zinazowakumba vijana wetu. Vijana ni wengi kuliko kundi lolote nchini na hawana
uhakika wa maisha yao ya kila siku hivyo wanahitaji kubadilika.”
Mwana-diplomasia
huyo mkongwe nchini ameendelea kusema kwamba maamuzi ya Serikali ya Tanzania kuelekea
kuwa Taifa la viwanda yatahamasisha vijana kupenda kujishughulisha na kazi
mbalimbali za uzalishaji kama vile kilimo.
“Jambo
la msingi kwa Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweka mazingira mazuri na rafiki
kwa vijana kuvutiwa katika sekta mbalimbali kwani nchi yetu inayo ardhi ya
kutosha tofauti na nchi nyingine barani Afrika. Lakini pia napenda kuchuku
fursa hii kuwaasa vijana kuchangamkia fursa hiyo kwani ni mtaji mkubwa kwao
katika kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.”
“Serikali
ya Awamu ya Tano imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba malighafi zote zinapata
masoko katika viwanda, miundombinu ya uhakika. Aidha, hii itachochea uzalishaji
na ajira kuongezeka maana bidhaa zote zitaongezwa dhamani hapa nchini badala ya
kuagiza nje bidhaa zilizoongezwa thamani na kudidimiza uchumi wa nchi yetu.”
Amesisistiza Dkt Salim.
Akitoa
Mfano wa athari za vijana kutojua historia yao Dkt Salim amesema Afrika ya Kusini
ni moja kati ya nchi za Afrika amabazo vijana wake wamekata tamaa na
kutowathamini Wazee walioshiriki katika harakati za kuleta ukombozi. Amesema, kitendo
hiki cha kuwadharau wazee kimepelekea mfarakano kati ya makundi haya mawili
ambayo yanawajibu mkubwa wa kushirikiana na kuijenga Afrika ya Kusini yenye
neema kwa wananchi wake wote bila kubagua.
Ameeleza
kwamba vijana hao wamejenga chuki na kuwachukia vijana wenzao waliotoka katika
nchi nyingine za Afrika na kuwaona maadui kwa kwenda nchini mwao na kufanya
kazi ambazo wao wanadhani ni za kwao. Athari hii inajitokeza kwa kuwa hawajui
historia ya nchi yao na nini viongozi wao walipigania katika kuweka misingi ya
umoja, amani na mshikamano Barani Afrika.
Hata
hivyo siwalaumu vijana hata kidogo kwa hakika vijana wana hali ngumu ya maisha kweli
kweli, wanahangaika kutafuta riziki, bila mafanikio. Ni vema kukaa nao na
kuongea kuhusu hali zao za maisha na changamoto zinazowakabili kwa pamoja
kutafuta ufumbuzi wa changamoto husika.
Bara
la Afrika lina changamoto nyingi, kama za uongozi, vita vya madaraka, makundi
yanayohamisiana, vita vya wenyewe kwa wenyewe , ukabila na mengineyo ambayo
hayaleti picha nzuri kwa Afrika na yanadhoofisha ustawi wa Bara letu na vijana
kukata tamaa.
Taasisi
ya Mwalimu Nyerere ina jukumu la kutoa elimu kwa vijana wote Barani Afrika juu
ya mustakabali wao na kuweka misingi imara ya umoja, amani, mshikamano
na Maendeleo kwa watu wote katika nchi zao bila kubaguana.
Tunaendesha
makongamano, midahalo na semina katika majukwaa mbalimbali ili kuwaelimisha vijana
kuhusu historia za nchi zao , viongozi wao na misingi waliyoiweka na umuhimu wa
kutanzua kwa pamoja changamoto zilizopo na kuongea yale yote ambayo wanadhani
hayaendi vizuri.
Dkt.
Salim amewomba vijana kuzingatia elimu wanayopewa maana Taasisi ya Mwalimu
Nyerere inahitaji kupata viongozi miongoni mwa vijana wa Tanzania. Ni vema
kujua changamoto zilizopo ili vijana hao watakaochukua uongozi kuendelea
kuelezea, kufundisha, kuuisha katika misingi ya umoja, amani, mshikamano na maendeleo
kwa watu wote na pia ustawi wa Mataifa yote ya Afrika.
Akizungumzia
suala la uongozi na ushiriki wa vijana katika kujenga Taifa, Dkt Salim amesema
ni vema vijana kushirikishwa katika uongozi kwa kuwa bado wana nguvu ya kuleta
maendeleo katika nchi zao. Hata hivyo alitoa tahadhari na kusema “Kijana sio
kigezo cha uongozi hata kidogo”,
Akitoa
mfano Dkt Salim amesema, “Mimi niliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Misri nikiwa na miaka 22, nadhani ni umri mdogo
kuliko vijana wa sasa wanaoteuliwa,
lakini niliaminiwa na kutimiza wajibu wangu kwa nchi na viongozi wangu
walioniteua, kwa kuwa nilijua tulikotoka, tulipo na tunakotaka kuelekea. Hayo
nilijifunza kutoka kwa viongozi wangu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee
Abeid Amani Karume.”
Dkt
Salim muda wote wa uongozi kama Balozi na mwakilishi wa nchi kimataifa alielezea
msimamo, matakwa na mapendekezo tunayokubaliana nayo kimataifa. Aidha,
alisisitiza suala la umoja, amani, mshikamano na jinsi ya kuleta maendeleo
katika nchi zote za Afrika kwa kuwa nchi yetu inaona bila umoja hakuna
suluhisho la amani katika nchi zetu na alifanya hayo kwa kuwa nilijua historia
ya nchi yangu.
“Wito
wangu kwa vijana ambao watakuja kuiongoza Taasisi ya Mwalimu Nyererer ni vema wakajipanga
kwa kuwa kazi iliyopo mbele yao ni kuwaelimisha vijana wenzao ili kuthamini na
kuuisha umoja, amani na kuleta maendeleo kwa watu wote iwe ni sehemu ya maisha
yao.”
Baba
wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume ni mfano wa kuigwa
katika kudumisha umoja, amani na mshikamano katika Bara la Afrika. Umoja wao
ulizaa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Dkt. Salim alimalizia kwa kusema
Mwalimu Nyerere siku zote za maisha yake, alikuwa akitembea na kuwaasa Watanzania
juu ya umoja, aman, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi. Mwalimu
alitambua wajibu wake.
Akitoa
hitimisho Dkt Salim amesema: “Hapa Tanzania asilimia 60 ya idadi ya watu
milioni 50 ni vijana, hawa wasipoelewa na kuuisha misingi ya Taifa lao yaani
umoja, amani, mshikamano na Maendeleo kwa watu wote bila ubaguzi tutakuwa
tumefanya kosa kubwa sana na dunia itatulaumu kwa hilo, kwa sababu Tanzania
ndio mfano wa kuigwa.”
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇