Mtwara
UZALISHAJI katika kiwanda
cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara umeathirika kwa kiasi kikubwa tokea
wiki iliyopita. Tatizo hili la muda limetokana na hitilafu za kiufundi katika
mitambo ya kiwanda. Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dangote Tanzania, Bwana Harpreet
Duggal amesema mafundi wa Dangote wapo kazini na shughuli za uzalishaji zitarejea
katika siku chache zijazo.
Alisema kiwanda kilianza
uzalishaji wa kibiashara mapema mwaka huu na kama ilivyo kwa kiwanda kingine
kama hicho jambo lolote linaweza kutarajiwa hasa katika miezi ya mwanzo. Hata
hivyo alizitaja hitilafu hizo kuwa ni za kawaida na uzalishaji utarejea katika
kipindi kifupi kijacho.
Alipoulizwa kuhusu gharama
kubwa za uzalishaji, Bwana Duggal alisema unapolinganisha na gharama nyingine
za uzalishaji katika Dangote, gharama za uendeshaji Tanzania ni za juu mno.
Moja ya sababu kuu ni matumizi ya jenereta za dizeli katika kuendesha kiwanda.
Na pia kiwanda kuwepo mbali na soko kuu la saruji kumechangia ongezeko la
gharama za usafirishaji. Akasema serikali inaangalia suala hili la gharama na jinsi
ya kutafuta njia ya kutupunguzia mzigo huu.
Akaongeza, “Tuna matumani
makubwa kuhusu uwekezaji wetu wa muda mrefu hapa Tanzania na tupo makini, kwa
kushirikiana na Serikali tutaweza kuhimili gharama za uzalishaji ili tuweze
kuendelea kufanya bidhaa ya saruji kuwa na
bei nafuu nchini.”
Tangu kuzinduliwa kwa
kiwanda cha saruji cha Dangote, bei ya saruji nchini Tanzania imeshuka kwa
zaidi ya asilimia 30.
Kiwanda cha Dangote
kilichopo Mtwara chenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 600 kina
uwekezaji mkubwa katika saruji kuliko vyote katika Afrika Mashariki. Kina uwezo
wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kutoa ajira ya moja kwa moja kwa
zaidi ya watu 1000 wa Mtwara.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇