Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewaalika
wafanyabiashara wa Cuba na Serikali ya nchi hiyo kuja hapa nchini kuwekeza
katika uzalishaji wa sukari na kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu.
Rais
Magufuli ametoa mwaliko huo leo tarehe 30 Agosti, 2016 Ikulu Jijini Dar es
Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Cuba hapa nchini Mhe.
Jorge Lopez Tormo.
Dkt.
Magufuli amemhakikishia Balozi Jorge Lopez Tormo kuwa Serikali yake itatoa
ushirikiano wa kutosha endapo mfanyabiashara yeyote wa Cuba au Serikali yenyewe
ya Cuba itajitokeza kuwekeza katika uzalishaji wa sukari na utengenezaji wa
dawa za binadamu, na kwamba licha ya Tanzania kuwa na mahitaji makubwa ya
bidhaa hizo kuna nchi nyingi jirani na Tanzania zitanufaika.
"Mhe.
Balozi ukiniletea huyo mwekezaji hata kesho nitamkabidhi shamba la kuzalisha
miwa na kujenga kiwanda cha kuzalisha sukari mara moja ili uzalishaji uanze,
tunataka kumaliza tatizo la sukari, uzalishaji wa sasa wa sukari hautoshelezi
mahitaji yote ya Tanzania na pia majirani zetu wana upungufu wa sukari"
Amesema Rais Magufuli na kuongeza kuwa yapo maeneo mengi yanayofaa kwa kilimo
cha miwa likiwemo eneo la Bagamoyo ambako kuna hekta takribani 10,000.
Hali
kadhalika Rais Magufuli amesema Serikali ipo tayari kutoa ardhi kwa mwekezaji
yeyote kutoka Cuba atakayekuwa tayari kujenga kiwanda cha kutengeneza dawa za
binadamu na vifaa tiba hapa nchini.
Kwa
upande wake Balozi Jorge Lopez Tormo amempongeza Rais Magufuli kwa juhudi kubwa
anazozifanya katika uendeshaji wa Serikali na amemhakikishia kuwa Cuba
itaendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri na wa kihistoria uliopo
kati yake na Tanzania, na ameahidi kufanyia kazi yote waliyoyazungumza.
Wakati huo huo,
Rais Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na Balozi wa India hapa Nchini
Mhe. Sandeep Arya ambapo Balozi huyo ametoa taarifa ya hatua zinazoendelea kuchukuliwa
baada ya ziara ya Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi iliyofanyika Mwezi
Julai mwaka huu.
Katika
mazungumzo hayo Balozi Sandeep Arya amesema wawekezaji kutoka India wanaendelea
na majadiliano na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) juu ya utekelezaji wa
mradi wa kusambaza gesi majumbani kwa ajili ya matumizi ya wananchi na pia
wanajadiliana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi juu ya kuongeza uzalishaji
wa mazao ya jamii ya kunde ili kulisha soko kubwa la mazao hayo nchini India.
Kuhusu
ujenzi wa kiwanda cha magari cha Tata, Balozi Sandeep Arya amesema mchakato unaendelea
na kwamba tayari wameoneshwa eneo la kujenga kiwanda hicho lililopo Kibaha
Mkoani Pwani na matarajio ni kuwa ujenzi wa kiwanda hicho utakamilika mwaka
ujao.
Kwa
upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na uwepo wa miradi hiyo
itakayoleta manufaa kwa pande zote mbili yaani Tanzania na India na ametoa wito
kwa pande zote kuharakisha majadiliano ili utekelezaji wa miradi hiyo uanze
haraka.
Aidha,
Rais Magufuli amewakaribisha wawekezaji wa India kuja kujenga hospitali kubwa
za matibabu ya binaadamu na kujenga viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu
huku akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu kwa
watanzania na wananchi wa nchi nyingine jirani na Tanzania wanaolazimika kusafiri
hadi nchini India kufuata matibabu.
"Wambie
wafanyabiashara wa India walio tayari kujenga hospitali kubwa, waje na mimi
nitawapa ardhi ya kujenga hospitali, wasipoteze muda waje sasa"
Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson
Msigwa
Kaimu
Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar
es Salaam
30
Agosti, 2016
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇