Ndugu Zubeir Ali Maulid
WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi
watokanao na Chama Cha Mapinduzi Zanzibar leo wamefanya Uchaguzi wa kumpata
mjumbe atakaye peperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Spika
wa Baraza hilo, kwa kipindi cha mwaka 2015 - 2020.
Taarifa kwa vyombo vya
habari iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC wa Idara ya Itikadi na Uenezi Mhe.
Waride Bakari Jabu, amesema uchaguzi huo ulioendeshwa na Mjumbe wa Kamati
Kuu ya CCM Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, ulifanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui,
Mjini Unguja.
Mwenyekiti wa Uchaguzi
huo, uliojumuisha wajumbe 72, alimtangaza
Zubeir Ali Maulid kuwa mshindi baada ya kupata kura 55 na kuwashinda wapinzani wake wawili aliyemaliza muda wake Pandu
Ameir Kificho aliyepata kura 11 na
Jaji Janeth Nora Sekihola aliyepata 4,
na kura mbili (2) ziliharibika.
Jumla ya wanachama wa tisa (9) walijitokeza kuomba ridhaa ya
CCM ili wagombee nafasi hiyo ya Spika .
Katika kikao cha Kamati
Maalum kilichofanyika Machi 24, mwaka huu, Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, ilipitisha
majina matatu ikiwa ni pamoja na Pandu Ameir, Zubeir Ali Maulid na Janeth Nora
Sekihola, ambapo uchaguzi wake umefanyika leo.
Akitoa neno la shukrani,
Zubeir Ali Maulid, aliwashukuru wajumbe hao kwa imani yao kwake na kuwataka
wampe kila aina ya mashirikiano ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Naye aliyekuwa Spika wa Baraza
hilo Pandu Ameir Kificho, amekubali kushindwa na kumuahidi kumpa msaada wowote
atakaohitaji, iwapo atatakiwa kufanya hivyo.
Uchaguzi huo wa Spika
unatarajiwa kufanyika mara tu baada ya kuitishwa kwa Baraza jipya la
Wawakilishi.
KIDUMU
CHAMA CHA MAPINDUZI.
Imetolewa na:-
Waride B.
Jabu
Mkuu wa Idara ya Itikadi na Uenezi - CCM,
ZANZIBAR.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇