------------------------------------------------------
Mkutano
wa 8 wa Nchi Jirani wa Libya chini ya Uenyekiti wa Waziri wa Mambo ya Nje wa
Tunisia Mheshimiwa Khemales Jhinaoui umefanyika jijini Tunis Tarehe 22 Machi,
2016. Mkutano huo uliotanguliwa na Mkutano wa Ngazi ya Wataalamu uliofanyika
tarehe 21 Machi, 2016 uliohusisha nchi jirani za Algeria, Chad, Misri, Niger,
Sudan na Tunisia. Waalikwa wengine katika Mkutano huo walikuwa ni Mwakilishi
Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Martin Kobler, Mwakilishi
Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Libya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete, Katibu
Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) Mheshimiwa Nabeer Al-Arabi na
Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni wa Umoja wa Ulaya Mheshimiwa Helga
Schmidt.
Mkutano
huo wa siku moja ambao ulihudhuriwa kwa mara ya kwanza na Mwenyekiti wa Baraza
la Utawala na Waziri Mkuu wa Libya Mheshimiwa Fayez Al-Sarraj umepitisha tamko
la pamoja kuunga mkono juhudi za kuleta amani nchini Libya chini ya Mkataba wa Makubaliano
(Libya Political Agreement) uliotiwa saini huko Skhirat Morocco Desemba 17,
2015. Wamewataka wale wote ambao hawakusaini Mkataba huo kufanya hivyo mapema
iwezekanavyo.
Kupitia
Tamko hilo, nchi jirani za Libya zimeelezea wasiwasi wao juu ya kuzorota kwa
hali ya usalama na kushamiri kwa ugaidi kunakotokana na ombwe la kisiasa nchini
Libya, hali inayoathiri usalama wa nchi jirani. Kwa ajili hiyo, nchi hizo
zimeunga mkono jitihada za Mwenyekiti wa Baraza la Utawala na Kiongozi wa Libya
Fayez Sarraj za kuunda Serikali na kuanza kazi Shughuli zake katika mji mkuu wa
nchi hiyo Tripoli. Wamewataka Wabunge wa
Bunge wote kuungana na kupitisha pendekezo la Baraza la Mawaziri ili Serikali
iweze kuanza kazi zake.
Kuhusu
kupambana na ugaidi ndani ya Libya, nchi hizo zimepinga kwa kauli moja
shambulio lolote la kijeshi kutoka nje ya Libya na kusema kuwa athari zake
zitakuwa kubwa kwa wananchi na nchi jirani na Libya. Wametaka shambulio lolote
la kijeshi kutoka nje litokane na ombi la Serikali ya Libya na kwa kuzingatia
Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Akizungumza
katika mikutano huo, Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika, Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete ameunga mkono jitihada za nchi jirani na Libya kuungana kwa pamoja
kusaidia kutatua mgogoro huo. Amesisitiza kuwa Umoja wa Afrika unaunga mkono
Mkataba wa Amani wa Libya na hauna dhamira ya kuanzisha mchakato mwingine bali
kuongeza msukumo katika mchakato uliopo. Hivyo, ameungana nao kuwataka wale
wote ambao hawajasaini mkataba huo kufanya hivyo. Amesisitiza pia umuhimu wa
Bunge la Libya kukamilisha wajibu wake wa kuidhinisha Baraza la Mawaziri ili
Serikali mpya iweze kufanya kazi.
Amewakumbusha nchi jirani za Libya juu ya wajibu wao wa kipekee katika
kusaidia kumaliza mgogoro huo na amewaahidi ushirikiano wa Umoja wa Afrika
katika kufikia azma hiyo.
Pichani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia na Mwenyekiti wa Mkutano wa 8 wa Marafiki wa
Libya Mheshimiwa Khemales Jhinaoui akifungua Mkutano jijini Tunis.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇