Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dar es salaam.
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Mhe. Rais Dkt. Magufuli amemteua
aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
kwenye Serikali ya Awamu ya Nne Mahadhi Juma Maalim kuwa Balozi wa
Tanzania nchini Kuwait kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya
Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.
Vile vile Rais ameagiza Wizara
ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa
kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao
imeisha na kuwataka Mabalozi hao kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au
Mwandamizi aliyechini yao leo hii.
Mabalozi hao ni Bi Batilda Salha Buriani, aliyeko Tokyo, Japan, Dkt. James Alex Msekela, aliyeko Rome, Italia.
Kwa mujibu wa Balozi Sefue, Rais
pia amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza,
Bwana Peter Allan Kallaghe ambaye anarejea Wizara ya Mambo ya Nje,
Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa ambapo
atakapopangiwa kazi nyingine.
Balozi Sefue alisema kuwa hadi
sasa vituo vya Ubalozi ambavyo viko wazi ni London nchini Uingereza
kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. Kallaghe, Brussels nchini
Ubelgiji kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous Kamala kuchaguliwa
kuwa Mbunge, Rome nchini Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dkt.
James Alex Msekela na Tokyo nchini Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa
Bibi Batilda Buriani.
Vituo vingine vya Ubalozi
ambavyo viko wazi ni Kuala Lumpar nchini Malaysia, kufuatia aliyekuwa
Balozi Dkt. Aziz Ponray Mlima kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa na
Brasilia nchini Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Bwana
Francis Malambugi.
Wakati huo Balozi Sefue alisema kuwa Rais ametengua uteuzi wa Mhandisi Madeni Juma Kipande kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha
Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇