Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiambatana na Katibu Mkuu Wizara
ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile alipotembelea ofisi za Wizara ya
Fedha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipata ufafanuzi kutoka kwa
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile wakati wa ziara
hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiongea na uongozi wa Wizara ya Fedha.
……………………………………………………………………….
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa
Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amefanya ziara ya
kushtukiza katika Ofisi za Wizara ya Fedha leo Ijumaa tarehe 6 Novemba,
2015.
Katika ziara hiyo Mhe.Rais
alipata fursa ya kutembelea baadhi ya Ofisi za Wizara na baadae
kuzungumza na Viongozi wa Wizara ili kufahamu changamoto ambazo
zinaikabili Wizara ya Fedha.
Wakati akimkaribisha Mhe.Rais
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile
alimueleza kuwa Wizara ya Fedha inakabiliwa na changamoto kubwa
inayotokana na makusanyo ya mapato ya ndani. Miongoni mwa sababu ni
misamaha ya kodi, wafanyabiashara wengi hasa wakubwa kukwepa kodi,
makusanyo yasiyoridhisha ya maduhuli na kutokulipwa kwa kodi za majengo.
Aidha Dkt. Likwelile alishauri ni bora kuwekwa mifumo mizuri, ikiwemo
matumizi ya Tehama na EFDs.
“Pamoja na ziara yangu kuwa ni ya
kustukiza nimefurahi sana kukuta Viongozi wote wapo ofisini na
wanafanya kazi. Jambo hili limenipa faraja kubwa. Ziara yangu ya kuja
hapa nimejifunza na kujua changamoto zipi zinazowakabili”. Alisema Mhe.
Rais.
Nimesikia changomoto nyingi na
ninaagiza kuwa muhakikishe walipa kodi wakubwa wanalipa kodi na
kusimamia kikamilifu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili iweze
kukusanya kodi kikamilifu na si kuwabana wafanya biashara wadogo wadogo.
Mhe.Rais aliwataka Viongozi wa Wizara kufanya kazi kwa bidii ili kuvuka lengo.
Imetolewa na;
Msemaji wa Wizara ya Fedha
Ingiahedi C.Mduma
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇