Na Mwandishi Maalum, New York
Udhibiti wa silaha za nyukilia na tishio la mataifa mengine la kujilimbikiza silaha hizo limendelea kuchukua sehemu kubwa ya majadiliano katika duru za Umoja wa Mataifa.
Kwa mara nyingine tena mataifa yanayo miliki silaha hizo yameendelea kutetea uhalali wa kuwa nazo, huku zile ambazo hazina hasa nchi zinazoendelea, licha ya kuhimiza kuhakikishiwa usalama wao, kutaka kuanzishwa kwa kanda huru dhidi ya silaha hizo, pia zimesisitiza haki ya kufanya utafiti, kuzalisha na kutumia nguvu za nyukilia kwa matumizi ambayo ni salama.
Kwa siku mbili mfululizo ( jumanne na jumatano) nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, wamekuwa na majadiliano ya jumla kuhusu upokonyaji wa silaha zikiwamo silaha za nyukilia, silaha ndogo na nyepesi wakati wa Mkutano wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu upokonyaji wa silaha ( UNDC).
Mkutano huo ambao ulikuwa uanze rasmi siku ya jumatatu lakini ukashindikana kuanza siku hiyo baada ya wajumbe kushindwa kukubaliana juu ya ajenda za mkutano.
Akiungana na wazungumzaji wengine, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi, pamoja na kutoa wito wa kuanzishwa kwa kanda huru dhidi ya silaya za nyukilia, amesititiza udhiti wa silaha hizo kwa kile alichosema, bila kufanya hivyo mataifa mengi yatajiunga katika mbio za kutaka kujilimbikizia silaha hiyo na hivyo kuiweka dunia katika hatari kubwa.
Balozi Manongi, kama ilivyo kuwa kwa wasemaji wengine wengi, amesema Tanzania inaamini katika majadilianao ya pamoja kupitia Umoja wa Mataifa ambao anasema ndilo eneo ambalo linaweza kuwakilisha mawazo ya wengi na hatimaye kutoka na kauli ya pamoja kuhusu upokonyaji wa silaha za aina zote pamoja na kudhibiti usambaaji wake.
“ Wakati tukizihimiza nchi zenye silaha za nyukilia kutuhakikisha usalama wetu na vilevile kujizuia kutoa vitisho vya kutumia silaha hizo kwa kisingizio chochote au katika mazingira yoyote yale. Tunaka haki ya sisi mataifa yanayoendelea kuwa na fursa ya kufanya utafiti, kuzalisha na kutumia nguvu za nyukilia kwa matumizi salama” akasisitiza Balozi Manongi.
Katika mchango wake, Tanzania kupitia mwakilishi wake, imeelezea wasiwake wake kuhusu Kamisheni ya Upokonyaji silaha ambayo kwa miaka kumi na tano imeshindwa kuwasilisha mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mapendekezo ya aina yoyote ile.
Kushindwa kwa Kamisheni hiyo kuwasilisha mapendekezo yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kunatokana na mambo mengine kwa wajumbe wa Kamisheni hiyo kushindwa kufikia makubaliano yenye tija.
Na kwa sababu hiyo Tanzania imewataka wajumbe wafikie mahali waache tofauti zao na kuonesha utashi wa kisiasa. Huku ikisisitiza kwamba utashi wa kisiasa utaiepusha dunia na matumizi ya silaha za nyukilia, matumizi ambayo hata Mahakama ya Kimataifa imesema yatakuwa yanakwenda kinyume na Katiba ya Umoja wa Mataifa.
Balozi Manongi akawaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, Tanzania ina imani kubwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kama chombo muhimu chenye mamlaka ya kusimamia na kudhibiti shughuli au program za nguvu za nyukilia zinazolenga katika matumizi salama.
Your Ad Spot
Apr 10, 2015
Home
Unlabelled
TANZANIA: WENYE SILAHA ZA NYUKILIA TUHAKIKISHIENI USALAMA WETU
TANZANIA: WENYE SILAHA ZA NYUKILIA TUHAKIKISHIENI USALAMA WETU
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Post Top Ad
Your Ad Spot
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇