KUMUOMBA MH. RAIS
JAKAYA MRISHO KIKWETE ASIPITISHE
MUSWADA WA SHERIA
YA MAKOSA YA MTANDAONI, 2015
Mtandao
wa waandishi kupitia mitandao nchini, Tanzania
Bloggers Network (TBN) tunamuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr.
Jakaya Mrisho Kikwete kutumia mamlaka yake vyema kwa kutokupitisha muswada wa
Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 unaokandamiza uhuru wa mawasiliano mitandaoni.
Muswada
wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya
mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na kuweka utaratibu
wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kieletroniki na masuala
mengine yanayohusiana na hayo.
MUSWADA WA SHERIA YA MAKOSA YA
MTANDAONI, 2015
Umoja
huu (TBN) ulishtushwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kukubali
kupitisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015 kwa hati ya dharura
kitendo ambacho hakikutarajiwa kutokana na kuwa mitandao bado ni kitu kipya nchini
hivyo tulihitaji maridhiano na wadau na elimu kati ya raia na Serikali ili wengi
watambue yapi ni makosa kwa kutumia mitandao na yapi yanakubalika.
Kimsingi
TBN haipingi Tanzania kuwa na Sheria ya Makosa ya Mtandao bali inaiomba
Serikali kuwashirikisha wananchi na hasa wadau wa habari na wanamitandao ya
jamii ili kuridhiana kwa vipengele ambavyo vinaonekana kukandamiza uhuru wa
vyombo vya habari. Na hatimaye kutoka na sheria isiyo na viashiria kandamizi
juu ya uhuru wa kupata na pokea habari.
Hali
kadhalika tulishuhudia watetezi wa haki za binadamu pamoja na wawakilishi wa
watumiaji wa Mtandao wa intaneti nchini wakitoa sababu zenye uzito za kwanini
sheria hii isipite kwa hati ya dharura na kuhoji kwanini sheria hii ipite kwa
dharura bila ya kupata majibu.
Muswada
huu ambao kati ya makosa mengi uliyonayo kubwa moja wapo ni majukumu makubwa
aliyopewa Mkuu wa Kituo chochote cha Polisi kuwa na uwezo wa kupekuwa na
kuchukua vielelezo/data pale anaposhuku kuna suala la uhalifu unaohusu mtandao.
Swali ni kuwa kwanini polisi apewe mamlaka ya kumsulubisha mtuhumiwa katika
hatua ya mwanzo bila uthibitisho wa sahihi?
Mbali
na hapo, sisi kama waandishi ulimwenguni kote tunatakiwa kufuatilia maadili ya
kazi zetu. Maadili ya mwandishi yeyote yule ni kutunza usiri wa chanzo cha
habari yake pale inapotakiwa lakini katika sheria hii sisi kama bloggers, sheria hii inakiuka hili kwa
kutulazimisha kutaja vyanzo vya habari.
Kupitia
sheria hii, bloga yeyote yupo hatarini kutokana na kwamba sheria inaainisha ni
kosa la jinai kutoa ujumbe unaoweza kumuudhi mtu kihisia.
Aidha,
tunamuomba Mheshimiwa Rais pia asipitishe
Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013.
Muswada
huu unavinyima uhuru vyombo vya habari vinavyotangaza takwimu mbalimbali. Kama
ilivyo Ibara ya 7(4) ‘‘Chombo chochote
cha habari ambacho kinachapisha taarifa za kitakwimu za uongo au upotoshaji, au
kinatangaza kipindi chochote kinachohusu shughuli za ukusanywaji wa taarifa
ambayo imefanywa au inafanywa na Ofisi, na hatimaye kusababisha wananchi
wasishiriki kwenye shughuli hiyo ya ukusanywaji wa taarifa au wasishirikiane na
maafisa wa Ofisi, kinatenda kosa.’’
Hii
iki maanisha kuwa hata blog zetu ziko hatarini kuelekea katika kulazimika
kufanya kazi za kuisifia serikali na kutangaza takwimu zilizopitiwa na serikali
tu, jambo ambalo litaharibu ukuaji wa uhuru wa habari nchini.
Tunamkumbusha mwananchi wa kawaida anayetumia mtandao wa intaneti
kuwa hayuko salama kwani sheria hii inamlazimisha mtoa huduma wa mtandao kutoa
taarifa za wateja wake jambo ambalo linahatarisha uhuru wa kutoa na kupokea
habari.
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu
Ibariki Afrika
IMETOLEWA NA;
Chama cha Bloggers Tanzania (Tanzania
Bloggers Network-TBN)
04/03/2015.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇