MAKITIBU WAKUU
Kadhalika, Rais Jakaya Kikwete amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuteua wanne wapya na kuhamisha mmoja, uteuzi uliomuondoa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Charles Pallangyo.
Pallangyo sasa anakua Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, nafasi ambayo inatafsriwa kuwa adhabu, siku chache baada ya vyombo vya habari ikiwamo FikraPevu kuibua kashfa ya uhaba wa dawa katika hospitali kubwa za serikali.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi na uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa.
Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa walioteuliwa ni pamoja na Dkt. Donan Mmbando ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuchukua nafasi ya Pallangyo.
Katika uteuzi huo Dkt. Yohana Budeba anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dkt. Adelhelm James Meru ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Maliasili.
Kabla ya uteuzi wake, Dkt Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Budeba alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi Futakamba alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dkt. Meru alikuwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Rais Kikwete amemhamisha Bibi Maimuna Tarishi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria
Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi Mtendaji, Manispaa ya Bukoba amepanda na kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Severine Kahitwa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita anakuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dkt. Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro anahamishiwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amemteua Kanali (Mst) Joseph Simbakalia, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kuwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA kuchukua nafasi ya Dkt. Meru.
Uteuzi huo unaanza leo na Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014, Ikulu, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇