Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita akizungumza mara baada ya kupokea msaada kutoka PSPF
Amelia Rweyimamu, Muwakilishi wa PSPF makao makuu Dar es salaam akizungumzia lengo la kushiriki ujenzi wa maabara
Afisa Mfawidhi wa PSPF mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne akifafanua jambo
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Wawakilishi wa PSPF, na Waaandishi wa habari wakizungumza wakati wa hafla
Na Mathias Canal, kilolo
Mfuko
wa Penseni (PSPF) umechangia bati 200 zenye geji 28, kwa ajili ya
kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa, ili kukamilisha
adhma ya ujenzi wa maabara kwa shule za sekondari Wilayani humo.
Akizungumza
baada ya kupokea bati hizo,Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerald Guninita,
alisema kuwa hakutarajia kupokea zawadi kama hiyo pamoja na kwamba
alituma maombi PSPF, hivyo bati hizo zitatumika kwa kazi maalumu ya
ujenzi wa maabara Wilayani humo kufuatia agizo lililotolewa na Rais wa
jamhuri ya Muungano wa Tanzania, la kujenga maabara ambapo hadi kufikia
tarehe 30 Novemba ujenzi huo unatakiwa kuwa umekamilika.
Guninita
alisema kuwa kukamilika kwa maabara hizo kutahamasisha watoto wengi
kupenda masomo ya sayansi kwani watasoma kwa vitendo na uhakika zaidi,
huku akizungumzia ufaulu mzuri wa kidato cha nne mwaka jana ambapo
Halmashauri ya wilaya hiyo ilishika nafasi ya kwanza kimkoa huku ikiwa
imeshika nafasi ya tisa kitaifa.
"Ninawashukuru
PSPF kwa kujitolea bati hizi kwa ajili ya Wilaya yangu ya Kilolo,
naamini hakutakuwa na kigugumizi katika utekelezaji wa agizo la Rais
kwani wadau kama ninyi mnapojitolea sisi hatuna budi kushukuru na
kufanyia kazi inayokusudiwa ya ujenzi ndani ya muda mwafaka". Alisema
Guninita
Guninita
aliongeza kuwa Wilaya ya Kilolo ina jumla ya shule 20 za Sekondari
ambazo kwa asilimia kubwa ujenzi wa vyumba vya maabara umekamilika hivyo
kwa sasa wamejikita katika ujenzi wa meza.
Kwa
upande wake Amelia Rweyimamu ambaye ni Muwakilishi wa PSPF makao makuu
Dar es salaam, akizungumza wakati wa kukabidhi bati hizo alisema kuwa
PSPF inatambua umuhimu wa kuwepo kwa maabara hapa nchini hivyo ofisi
yake imeona vyema kushiri katika ujenzi huo kwa kutoa bati hizo.
Rweyimamu
alisema PSPF inatoa mafao mbalimbali ikiwa ni pamoja na fao la uzeeni,
fao la ulemavu, fao la kifo, fao la mazishi, fao la wategemezi lisilo na
kikomo, fao la kujitoa, fao la uzee, fao la kufukuzwa kazi, na fao la
ujasiriamali.
Aidha
aliongeza kuwa PSPF inatoa fao la elimu ambapo mfuko hudhamini mikopo
katika bodi ya mikopo ya wanafunzi, lengo kubwa ikiwa ni kujenga uwezo
wa kuhudumia wanafunzi wengi katika taaluma mbalimbali ikiwemo pia
taaluma ya sayansi, Teknolojia na Afya.
Naye
Afisa Mfawidhi wa PSPF mkoa wa Iringa, Baraka Jumanne, alisema kuwa
PSPF imetoa bati 200 kwa Wilaya ya Kilolo ambazo zina thamani ya
shilingi milioni sita za kitanzania ili kusaidia ujenzi wa shule
Wilayani humo.
Jumanne
alisema maabara ya sayansi ni muhimu katika maendeleo ya wanafunzi
kujifunza kwa nadharia na vitendo kutokana na umuhimu huo, kunahitajika
ushirikiano kama ule ulioonyeshwa wakati wa ujenzi wa shule za sekondari
za kata.
Hata
hivyo hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Jakaya
Kikwete, aliwaagiza wakuu wa mikoa na wilaya nchini, kujenga maabara kwa
kila shule ya sekondari katika kipindi cha miaka miwili, kuanzia sasa
ambapo alitoa agizo hilo wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo
la Manyoni Magharibi mkoani Singida, waliohudhuria mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Mji mdogo wa Itigi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇