Na Mwandishi wetu
Kituo cha Radio 5, kimepongezwa na wadau wa sanaa kwa mchango wake wa kukuza sanaa za vichekesho vya majukwaani hapa nchini.
Wadau hao wa sanaa za vichekesho vya majukwaani waliipongeza Radio 5, wakati wa burudani ya wachekeshaji wa majukwaani iliyofanyika mwishoni mwa wiki hii katika ukumbi wa Golden Tulip.
Burudani hiyo ambayo ilifana sana iliwajumuisha mchekeshaji kutoka Uganda, mwanadada Anne Kansiime, Fred Omondi kutoka Kenya na Pilipili wa Tanzania.
Akizungumzia onyesho hilo, mmoja ya mashabiki waliohudhuria onyesho hilo, amesema sanaa ya vichekesho vya majukwaani nchini haijapewa kipaumbele kama aina nyingine za sanaa.
‘Watu wengi bado wanaamini sanaa za kuchekesha majukwaani sio kazi rasmi kama kazi nyinginezo, lakini hii imeanza kubadilika hapa nchini, na tutarajie mabadiliko zaidi kama wadau wengine kama radio 5 wakijitokeza kusaidia’ alisema Farida Akida.
Akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na anavyoiona tasnia ya vichekesho vya majukwaani Afrika Mashariki, mchekeshaji Anne Kansiime anasema anaamini sanaa ya vichekesho vya majukwaani inaanza kujijengea heshima kubwa miongoni mwa wananchi.
‘Mimi sio mbunge au mwanasiasa, lakini nimepata mapokezi makubwa, kwa kazi hii tu ya kuchekesha watu, hivyo naona hii tu pekee ni dalili ya kukua kwa tasnia hii hapa Afrika Mashariki’ alisema Anne.
Ikiwa ni mara ya kwanza kwa mwanadada Kansiime kuja Tanzania kutoa burudani, hasa baada ya kujijengea umaarufu mkubwa kupitia vipande vyake vya vichekesho vilivyo mtandaoni, tiketi za burudani yake ziliisha wiki moja kabla hajawasili.
Katika usiku huo wa burudani ulioitwa, Cheka Kwa Nguvu, mchekeshaji toka Tanzania, Pilipili aliwatoa kimasomaso mashabiki waliofurika kwa vichekesho vyake vilivyoonekana kuwagusa mashabiki moja kwa moja.
Huku mashabiki wengi wakiwa hawamfahamu vyema, Pilipili ambaye kitaaluma ni mwalimu, anasema aliacha kazi ya ualimu ili awe mchekeshaji, hivyo kwake yeye, kuchekesha ni kazi kama kazi nyingine.
‘Kwangu mimi hii ni kazi ambayo najivunia, na naamini nitaweza kuwawakilisha watanzania vyema kimataifa kupitia uchekeshaji, na naishukuru Radio 5 kwa kunipa fursa ya kuonyesha kwamba ninaweza’ alisema Pilipili.
NayeMkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Radio 5, Robert Francis amesema huu ni mwanzo tu wa kuwaandalia watanzania burudani za kipekee na watarajie mengi zaidi kutoka Radio 5.
‘Sanaa ya uchekeshaji jukwaani bado haijapewa nafasi kubwa hapa nchini, lakini kama mlivyoona, mashabiki wamejitokeza kwa wingi sana kwenye burudani yetu, hivyo watu watarajie burudani za aina hii nyingi zaidi kutoka kwetu’ alimaliza Francis.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇